JKCI mshindi wa kwanza watoa huduma bora za afya
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Friday, Jul 17, 2026
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la watoa huduma bora za afya na tiba katika maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA).
Tuzo hiyo imetolewa jana na Waziri wa Kazi na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Shariff Ali Shariff wakati wa kufunga maonesho hayo jijini Dar es Salaam.
Baada ya kupokea tuzo hiyo baadhi ya wafanyakazi wa JKCI waliokuwa wakitoa huduma katika maonesho hayo waliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fursa kwa Taasisi za afya kushiriki katika maonesho hayo na kuwafikishia wananchi huduma karibu.
Dorothea Simkayi mfamasia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema huduma zilizokuwa zikitolewa katika maonesho hayo zinatolewa katika matawi yote ya JKCI hivyo wananchi waliopata huduma na kupewa rufaa ya kufanya uchunguzi zaidi wasisite kutembelea matawi ya JKCI yaliyopo karibu nao kwaajili ya uchunguzi zaidi.
“Katika maonesho ya mwaka huu tumeboresha zaidi huduma tunazozitoa, wananchi waliotembelea banda letu hawakutarajia kupata huduma tulizowapa lakini pia wale wote waliohitaji dawa zote walizipata hapa”, alisema Dorothea.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jackline Mwaipopo alisema wananchi waliopata huduma katika banda la Taasisi hiyo walinufaika na vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa urahisi pamoja na kkuzifahamu namba zao za afya.
“Kupitia kampeni ya Jua namba zako tumebaini kuwa wananchi wengi wanapenda kufanya uchunguzi wa afya lakini mara nyingi hushindwa kutokana na hofu ya gharama, JKCI inaendelea kutoa huduma hizi bila malipo hata baada ya maonesho ya SABASABA hivyo nawasihi wananchi waendelee kujitokeza katika matawi yetu yote ili wapate huduma za uchunguzi na ushauri wa afya”, alisema Jackline.