Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

JKCI yazindua mfumo wa kidijitali wa kufuatilia wagonjwa majumbani ujulikanao kama DOZEE mkoani Arusha

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jul 16, 2026
image description

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mhe. Paul Makonda ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza teknolojia za kisasa katika sekta ya afya.

Pongezi hizo alizitoa wakati akizindua huduma ya kuwafuata wagonjwa majumbani kwa kutumia shuka maalumu lijulikanalo kama DOZEE wakati wa kambi maalumu ya kupima na kutibu magonjwa ya binadamu inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.

Mhe. Makonda ambaye pia ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea kupiga hatua barani Afrika katika matumizi ya ubunifu wa kidijitali kuboresha huduma za matibabu ya moyo na kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Matumizi ya teknolojia katika usajili wa wagonjwa, utunzaji wa kumbukumbu za kitabibu na ufuatiliaji wa wagonjwa wakiwa wamelazwa na baada ya matibabu kwa kutumia shuka la DOZEE ni sehemu ya maono ya Serikali ya kujenga taifa lenye uchumi unaotegemea maarifa, sayansi na teknolojia”, alisema Mhe. Makonda

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema tekniolojia ya DOZEE ina uwezo wa kufuatilia viashiria muhimu vya afya kwa mgonjwa vinavyojulikana kitaalamu kama vital signs ikiwemo mapigo ya moyo, kiwango cha oksijeni kwenye damu na shinikizo la damu.

“Kwa lugha rahisi DOZEE ni mfumo unaotumia kifaa maalumu kinachowekwa chini ya godoro la mgonjwa na kufuatilia viashiria muhimu vya afya bila kulazimika kuunganisha vifaa vingi moja kwa moja kwenye mwili wa mgonjwa”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema taarifa za mgonjwa zinazokusanywa kupitia mfumo wa DOZEE zinaweza kumfikia daktari kwa njia ya kidijitali ikiwemo kupitia simu ya mkononi hivyo kumwezesha kufuatilia mwenendo wa afya ya mgonjwa hata akiwa nje ya hospitali au akiwa anaendelea na shughuli nyingine.

“Tunatumia teknolojia hii tukiwa na malengo ya kusaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika hususan vinavyotokea baada ya hali ya mgonjwa kubadilika ghafla akiwa nyumbani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini”, 

“Wagonjwa wanaporuhusiwa kwenda nyumbani hali zao zinaweza kubadilika ghafla, Shinikizo la damu linaweza kushuka, mapigo ya moyo yanaweza kwenda kwa kasi sana au kiwango cha oksijeni kwenye damu kikapungua. Kupitia teknolojia hii, daktari anaweza kupata taarifa kwa wakati na kuchukua hatua mapema kabla hali ya mgonjwa haijawa mbaya,” alisema Dkt. Kisenge.

Huduma hiyo ya DOZEE sasa kuanza kutumika kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).