Mhe. Makonda awahimiza wananchi wa Arusha kupima afya ya moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Tuesday, Jul 14, 2026
Wananchi wa Mkoa wa Arusha na Mikoa ya jirani wametakiwa kujitokeza kupima moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) linalotoa huduma bingwa bobezi za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Rai hiyo imetolewa leo na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mhe. Paul Makonda wakati wa kambi maalumu ya kupima na kutibu magonjwa ya binadamu inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.
Mhe. Makonda alisema JKCI ni Taasisi bora katika kutoa huduma bingwa bobezi za moyo Africa Mashariki na Kati hivyo wananchi watumie uwepo wa Taasisi hiyo kufanyiwa uchunguzi wa afya na kupata taarifa sahihi kuhusu afya zao.
“Msiposhiriki katika kambi hii kupata huduma bingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo hapo baadaye mkikutwa na magonjwa haya mnaweza kutumia mtaji wenu wote kwaajili ya kupata matibabu, ni muhimu sasa mkapima”, alisema Mhe. Makonda
Mhe. Makonda alisema JKCI wamefungua tawi lake mkoani Arusha kwaajili ya watu wa kanda ya Kaskazini hivyo wale wote watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo kupitia kambi hiyo watatibiwa katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre ambalo ni Tawi la JKCI.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge alisema JKCI imejipanga kuwahudumia watu wote wanaohitaji huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo hivyo wasisite kufika katika banda hilo kwaajili ya matibabu.
Dkt. Kisenge alisema kupitia kambi hiyo wataalamu mabingwa wabobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima wameshiriki kwa kutoa huduma lakini pia kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Tupo hapa madaktari wa kutosha kutoka JKCI makao makuu na JKCI Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), lengo letu ni kuhakikisha kuwa huduma za matibabu ya moyo zinawafikia wananchi wote”, alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI tawi la Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inaenda kuzindua huduma ya kuwafuata wagonjwa majumbani kwa kuwawekea kifaa maalumu kinachojulikana kwa jina la DOZEE ambacho kinawekwa chini ya godoro la mgonjwa akiwa nyumbani na kuweza kusoma shinikizo la damu, kiwango cha hewa mwilini, mapigo ya moyo na umeme wa moyo.