Watu 1,200 wafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo maonesho ya SABASABA
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Friday, Jul 17, 2026
Watu 1,200 waliotembelea maonesho ya 50 SABASABA wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kupata elimu kuhusu magonjwa hayo.
Uchunguzi huo ulifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA) yaliyofanyika kwa siku 16 katika viwanja vya Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuhitimisha maonesho hayo jijini Dar es Salaam Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Thabiti Ramadhani alisema mwitikio wa wananchi kufahamu afya zao ulikuwa mkubwa ambapo watu 510 walijitokeza kujua namba zao za afya.
“Watu wengi waliofika hapa hawakuwa wanajua kama wana matatizo ya kiafya kupitia kampeni yetu ya “Jua Namba Zako” tumeweza kubaini asilimia 75 ya watu waliojitokeza wana matatizo ya kiafya bila wao kujua ambapo wengi wamegundulika kuwa na kisukari, shinikizo la juu la damu, uzito mkubwa na magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Thabiti.
Dkt. Thabiti aliongeza kuwa ni muhimu wananchi kutumia fursa zinazopatikana wakati wa maonesho kama ya SABASABA kujitokeza kupima afya zao kwani huduma hizo huokoa muda na gharama.
“Katika maonesho haya tulikuwa tukitoa huduma za kupima utendaji wa moyo kwa kutumia mashine ya ECG (Electrocardiography) na kuangalia mfumo wa umeme unavyofanyakazi kwa kutumia machine ya ECHO (Echocardiogram) pamoja na kuangalia utendaji wa moyo wakati wa mazoezi (Stress test) na wale waliogundulika kuwa na matatizo walipatiwa matibabu na wengine kupewa rufaa”, alisema Dkt. Thabiti
Aidha Dkt. Thabiti aliwataka wananchi kuzingatia lishe bora ili kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza huku akisistiza umuhimu wa kupima homa ya ini na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo.
“JKCI tunatoa huduma za kupima homa ya ini na chanjo yake ambapo katika maonesho haya watu 50 walijitokezaa kupima ugonjwa huo”, alisema Dkt. Thabiti.