Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

JKCI yapongezwa kwa kuanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Saturday, Jul 11, 2026
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepongezwa kwa kuanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuweka jiwe la msingi la Taasisi hiyo tawi la Temeke.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyofanyika jana katika Tawi la JKCI Hospitali ya Dar Group iliyopo Tazara jijini Dar es Salaam.

Prof. Mkumbo alisema hatua ya uwekaji wa jiwe hilo la msingi inaenda sambamba na maandalizi ya ujenzi wa jengo litakalokuwa likitoa huduma za tiba ya michezo kwaajili ya maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 ambapo Tanzania ni mwenyeji wa michuano hiyo.

“Uwekezaji huu muhimu unaenda kukuza na kuhamasisha utalii tiba nchini kwani utawasaidia watalii wanaokuja Tanzania kupata huduma bora za afya katika taasisi zetu za afya ikiwemo JKCI”, alisema  Prof. Mkumbo.

Prof. Mkumbo alisema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita JKCI imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 37 ambazo zilikuwa zikitumika kuwapeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi kwaajili ya matibabu.

“Taasisi hii imekuwa ikishiriki katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa kuokoa fedha nyingi ambazo kwa sasa zinaelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo”, alisema Prof. Mkumbo.

Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi alisema uwekezaji wa jengo la tiba ya michezo utasaidia kutoa huduma muhimu za uchunguzi na matibabu kwa wanamichezo ikiwa ni hatua za kimkakati kuelekea AFCON 2027.

“Tunafungua ukurasa mpya wa huduma za moyo nchini kwa kuweka kituo muhimu kitakachotoa huduma za kinga, uchunguzi na ushauri wakitalaamu kwa wananchi na wanamichezo ili waweze kushiriki na kufurahia mashindano ya AFCON 2027 kwa usalama unaozingatia viwango vya kimataifa”, 

“Tunamshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya afya ikiwemo vifaa tiba, mafunzo kwa watalaamu wa afya yote ili huduma bingwa ziwafikie wananchi kwa karibu”, alisema Dkt. Florence

Dkt. Florence alisema JKCI ina dhamira ya dhati ya kusogeza huduma karibu na wananchi kwani kuanzishwa kwa tawi la Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kumepanua wigo wa huduma za dharula za moyo kwa wananchi na watalii wanaotembelea nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema uwekezaji huo wenye thamani ya shilingi bilioni 18 utaifanya JKCI kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa huduma za Kibingwa na ubingwa bobezi katika tiba ya moyo pamoja na huduma nyingine maalumu kwa viwango vya kimataifa.

“Jengo hili litakuwa la pili kwa ukubwa barani Afrika katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo pamoja na huduma za tiba ya michezo (Sport Medicine) hivyo kuchochea wanamichezo kutoka mataifa mbalimbali kuja kupata huduma JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.

Katika hatua nyingine Dkt. Kisenge alisema kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza JKCI imeanzisha kampeni ya Jua Namba Zako yenye lengo la kuhamasisha wananchi kutambua hali zao za afya na kuokoa Maisha.

Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI imeendelea kuwafikia wananchi kupitia huduma za tiba mkoba ambapo hadi sasa mikoa 23 imefikiwa na kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo na mishipa ya damu, pia kufikisha huduma hizo katika nchi jirani ikiwemo Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Zambia na Visiwa vya Comoro.