JKCI na BMH waimarisha utalii tiba, wafanya upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka nchini Burundi
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Jul 11, 2026
Watoto kutoka nchini Burundi waliokuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na watalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) hatua inayoendelea kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba Barani Afrika.
Upasuaji huo umefanyika katika kambi maalumu yenye malengo ya kuweka ushirikiano baina ya wataalamu hao, kubadilishana ujuzi pamoja na kuonesha umahiri wa wataalamu wa Tanzania katika kutoa huduma bingwa bobezi za upasuaji wa moyo kwa watoto.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi alisema mafanikio ya kambi hiyo yameonesha uwezo wa wataalamu wa Kitanzania kutoa huduma za kibingwa kwa kushirikiana huku ikidhihirisha matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya.
Prof. Makubi alisema kambi hiyo ni mwanzo wa ushirikiano kati ya BMH na JKCI ukiwa na dhumuni la kuongeza upatikanaji wa huduma za magonjwa ya moyo kwa watanzania na watu kutoka katika mataifa mengine.
Aidha Prof. Makubi alisema kambi hiyo imeandika historia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kuwa mara ya kwanza kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka nje ya Tanzania jambo linaloonesha mafanikio ya utekelezaji wa mkakati wa tiba utalii nchini.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa Watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema ushirikiano huo umeiwezesha timu za wataalamu wa upasuaji wa moyo kubadilishana uzoefu na kuongeza uwezo wa kutoa huduma za kibingwa.
“Tumefurahia sana kupata mwaliko kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kuungana nao kutoa huduma ya upasuaji wa moyo kwa watoto waliotoka nchini Burundi, tunaziomba na Hospitali nyingine nchini zishirikiane nasi lengo likiwa ni kuongeza ujuzi na kuokoa maisha ya watoto wanaohitaji huduma za upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Godwin.
Naye Mratibu wa Utalii Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita alisema mafanikio ya kambi hiyo yanaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tiba utalii Barani Afrika.
“Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inataka Tanzania kuwa kitovu cha tiba utalii Barani Afrika, leo tumejionea ushirikiano wa hospitali zetu hizi mbili zilivyoanza kutekeleza maono hayo kwa vitendo”, alisema Dkt. Asha
Akitoa neno la shukrani daktari kutoka nchini Burundi Nzitunga Octavie alisema familia za watoto waliopatiwa matibabu katika kambi hiyo wameshukuru kwa ukarimu wa watanzania kuanzia mapokezi yao hadi huduma walizopatiwa.
“Tulipofika hapa tulijisikia kama tuko nyumbani tunashukuru sana madaktari wote waliofanya upasuaji wa moyo kwa watoto wetu kwani tunaamini baada ya matibabu waliyoyapata watapona”, alisema Dkt. Octavie
Dkt. Octavie alisema kupitia kambi hiyo ameweza kujifunza mambo mengi ya kitaalamu yanayohusu magonjwa ya moyo kwa watoto kwa kufanya kazi na wataalamu wa Tanzania katika kutoa huduma kwa watoto waliotoka nchini Burundi.