China kutumia shilingi bilioni 112 kujenga Jengo jipya la JKCI Mloganzila
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, May 25, 2026
Serikali ya Watu wa China kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) kujenga jengo lenye thamani ya shilingi bilioni 112 katika eneo la Mloganzila kwaajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto.
Jengo hilo linalotarajiwa kuhudumia takribani watoto 900 ni sehemu ya malengo ya kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo kwa kuboresha upatikanaji wa huduma na kupunguza foleni ya watoto wanaohitaji huduma za upasuaji wa moyo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya wahandisi kutoka Jamhuri ya Watu wa China Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kwa sasa Taasisi hiyo ina uwezo wa kuhudumia watoto 400 wanaohitaji upasuaji wa moyo hivyo uhitaji wa nafasi kwaajili ya kutoa huduma bado unahitajika.
“Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alikutana na Rais wa China Xi Jiping wakakubaliana kujenga jengo jipya la JKCI ambalo litagharimu kiasi cha shilingi bilioni 112, hatua hii inatokana na ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa na Taasisi yetu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema jengo hilo litatoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za maabara, chumba maalumu cha upasuaji wa moyo (Theater), na Cathlab kwaajili ya upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo.
Aidha Dkt. Kisenge alibainisha kuwa kwa sasa JKCI inapokea watoto zaidi 16000 kwa mwaka ambao wanahitaji uchunguzi, matibabu na upasuaji wa moyo kwa haraka hivyo ni muhimu kupata jengo jingine litakaloweza kusaidia matibabu hayo na kupunguza msongamano uliopo.
“Tunatarajia jengo hilo linaloanza kujengwa kuanzia mwezi ujao litapunguza idadi ya vifo vya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaochelewa kupata huduma ya upasuaji hivyo kuokoa maisha yao”, aliasema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Ubalozi wa China Nchini Tanzania Yang Zeyu alisema urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na China umewezesha ushirikiano katika kujenga jengo hilo la matibabu ya moyo kwa watoto ili kuwasaidia watoto wengi zaidi kupata matibabu kwa wakati.
“Ushirikiano katika sekta ya afya kati ya China na Tanzania ni wa miaka mingi, tumekuwa tukileta watalamu wetu ili waweze kuongeza nguvu ya kuwahudumia wagonjwa hapa Tanzania, mradi huu utaanza haraka iwezekanavyo ili watoto wa Tanzania waweze kupata huduma za haraka na kupunguza muda wa kusubiria huduma”, alisema Zeyu.
Naye Mkuu wa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoka Jamhuri ya Watu wa China Yang Ling alisema Serikali ya China imedhamiria kushirikiana kimkakati na Tanzania katika sekta ya afya kwa kuleta wataalamu na kuimarisha miundombinu pamoja na vifaa tiba.
“Jengo tutakalolijenga litakuwa ni jengo la kisasa, na kuweka miundombinu ya kutoa huduma zote katika jengo hilo ili watoto watakapofikishwa hapo waweze kupata huduma zote”, alisema Yang.