Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Kampeni ya Jua Namba Zako yawafikia Maafisa Utawala na Rasilimali Watu nchini

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, May 06, 2026
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yafikisha kampeni ya Jua Namba Zako kwa maafisa Utawala na Rasilimali Watu wanaoshiriki Mkutano Mkuu wa pili Jumuishi wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma Tanzania. 

Kupitia Mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) JKCI inatoa huduma za uchunguzi wa viashiria vya magonjwa ya moyo kwa wataalamu hao huku ikitoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.

Akizungumza jana wakati wa mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imetoa elimu kuwahimiza maafisa Utawala na Rasiliamli Watu nchini kupima afya zao mara kwa mara na kujua namba zoa za afya.

“Lengo letu kuu ni kuihamasisha jamii kujua namba zao, kupima na kuchukua hatua, haya yote yatatimia kama jamii itapima shinikizo la damu, uzito, urefu, sukari katika damu, mapigo ya moyo na mafuta katika damu kwani vitu hivi vinachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo” alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge aliwaambia maafisa Utawala na Rasilimali Watu wakijua namba zoa mapema watajizuia kupata maathiriko makubwa yanayoweza kujitokeza na kuathiri utendaji kazi wao.

“Sambamba na malengo ya mkutano huu, kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto, na kuboresha utendaji kazi katika sekta ya umma pia tumieni muda huu kujua namba zenu kwani JKCI tunataka kuhakikisha tumepunguza idadi ya watu wanaopata magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge 

Kwa upande wake Afisa Utumishi Mkuu kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba Rosada Mbowe aliwashukuru wataalamu wa JKCI kufikisha huduma hizo katika mkutano huo kwani umetoa fursa kwao kupima afya zao.

Rosada alisema kutokana na yeye kuishi Bukoba ingekuwa ngumu kwake kufika JKCI kufanya uchunguzi kama ambao amefanyika, labda ingemlazimu kufanya vipimo hivyo kama angekutana na changamoto za kiafya.

“Utaratibu huu wa kuchunguza afya kabla ya kuumwa ni mzuri, inatubidi tuwe tunafanya hivi mara kwa mara kwani inakuweka kuwa salama, unajijua vizuri na kuchukua hatua mapema kutokana na ushauri wa wataalamu wa afya”, alisema Rosada

Naye Afisa Utawala kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Muguha Titus Muguha alisema amekuwa na utaratibu wa kupima shinikizo la damu mara kwa mara hivyo akaona ni wakati sasa kukutana na wataalamu wa JKCI kupata uhakika wa vipimo hivyo.

 “Mambo ni mengi na maisha yamebadilika, ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya ikiwezekana JKCI iandae waraka wa kushauri uongozi wa juu watumishi wa umma iwe ni lazima kufanya vipimo hivi kwani itasaidia kuboresha afya za watumishi wa umma na kulinda nguvu kazi ya Taifa”, alisema Mugaha

Mugaha alisema ikiwa lazima kwa watumishi wa umma kupima na kujua namba zao hata jamii itachukua hatua ya kupima na kujua namba zao lakini pia watumishi watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha familia zao nazo zinapima na kujilinda na magonjwa ya moyo. 

“Magonjwa haya sio tu yanaigharimu Serikali bali pia yanazigharimu hata familia zetu kwani inapotokea familia ikakutana na changamoto za magonjwa ya moyo nguvu kazi katika familia inapungua, kipato cha familia kinaelekezwa katika kupata matibabu na kusababisha uchumi wa familia kushuka”, alisema Mugaha.