Wafanyakazi JKCI Dar Group wapewa onyo dhidi ya ubadhilifu wa mali za Umma
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, May 06, 2026
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wametakiwa kuepuka ubadhilifu katika matumizi ya mali za umma ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya ofisi pamoja na vitendo vya uhujumu uchumi vinavyoweza kuathiri utendaji wa kazi za taasisi.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa JKCI Hospitali ya Dar Group, Dkt. Tulizo Shemu wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo kwa wafanyakazi bora ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani.
Dkt. Shemu alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kutumia kwa uangalifu rasilimali za ofisi ili kupunguza upotevu wa fedha za umma na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“Wewe Mfanyakazi usiwe chanzo cha upotevu wa mali za umma, epuka kununua vifaa vya ofisi kwa gharama zisizo na sababu na hakikisha unavitunza vizuri vifaa vyote vilivyonunuliwa.Ukibainika kufanya ubadhilifu au matumizi mabaya ya mali za umma hatua za kinidhamu zitachukuliwa ikiwemo kufikishwa TAKUKURU”, alisema Dkt. Shemu.
Dkt. Shemu alisema kila mfanyakazi ana jukumu la kufanya kazi kwa bidii na kuepuka uzembe ili kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa na kuongeza kuwa uhujumu uchumi hauhusiani tu na wizi wa fedha bali pia ni pamoja na kupokea mshahara bila kufanya kazi ipasavyo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Rasilimali Watu wa JKCI Hospitali ya Dar Group Neema Minja, aliwapongeza wafanyakazi kwa ushirikiano mzuri kazini na kuwataka kuongeza juhudi katika kuwahudumia wananchi kwa upendo na weledi.
“Licha ya baadhi ya wafanyakazi kupata zawadi za wafanyakazi hodarileo, nawasisitiza na nyie wengine kujituma kazini na kufanya kazi kwa upendo ili wagonjwa waendelee kufurahia huduma zetu”, alisema Neema.
Nao baadhi ya wafanyakazi waliochaguliwa kuwa wafanyakazi hodari wa mwaka wa fedha 2025/26 walisema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za pamoja na ushirikiano kazini.
Kwa upande wake Mhandisi wa Vifaa Tiba JKCI Dar Group Elpidius Prosper ambaye ni mfanyakazi hodari wa hospitali hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 alisema ushindi huo ni motisha ya kuongeza juhudi zaidi kwani wafanyazi wote ni bora katika nafasi zao hivyo basi wafanye kazi kwa bidii ili wananchi waendelee kunufaika na huduma wanazozitoa.
“Kuchaguliwa kwangu kuwa meneja Tuzo hii ni matokeo ya mshikamano wa wafanyakazi wote kwani kidole kimoja hakivunji chawa hivyo basi tuendelee kushirikiana kwa bidii kwani kufanya kazi kwa pamoja kunaifanya taasisi yetu ifike mbali zaidi”, alisema CPA. Ashura Ally, Meneja wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa JKCI Dar Group ambaye amechaguliwa kuwa meneja hodari wa mwaka wa fedha wa 2025/26.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa JKCI Dar Group, John Owenya ambaye amechaguliwa kuwa Mkuu wa Kitengo hodari wa mwaka wa fedha 2025/26 alisema mafanikio ya kazi yanatokana na bidii na uwajibikaji wa kila mmoja aliwahimiza wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi na matokeo yake yataonekana na watu kuridhika na huduma unazozitoa.