Wafanyakazi JKCI Watakiwa Kujituma Ili Kuongeza Kipato Chao
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Tuesday, Apr 28, 2026
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, kwa weledi na kwa ubunifu zaidi ili kuongeza uzalishaji na mapato ya taasisi, hatua itakayowezesha kila mmoja kujipatia kipato kinachoendana na juhudi na mchango wake katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kumi wa Baraza la Wafanyakazi wa taasisi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo alisisitiza kuwa taasisi hiyo imeingia katika mfumo mpya wa utendaji unaolenga kulipa wafanyakazi kulingana na bidii, uwajibikaji na matokeo ya kazi zao.
Dkt. Kisenge alisema mfumo huo mpya utasaidia kuongeza ari ya kazi, ushindani chanya na uwajibikaji kwa wafanyakazi wote huku kila kurugenzi ikitakiwa kubuni mikakati ya kuongeza mapato kwa kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
“Huu ni mkakati mpya katika taasisi yetu ambapo mfanyakazi atalipwa kulingana na bidii yake ya kazi. Hivyo ninawaomba wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii ili mjipatie kipato kitakachowasaidia kuboresha maisha yenu”, alisema Dkt. Kisenge.
Alisema kaulimbiu ya taasisi kwa sasa ni “Wafanyakazi Kwanza” inayolenga kuhakikisha wafanyakazi wanaojituma wanapata stahiki zao kwa haki, huku akibainisha kuwa haitakuwa rahisi tena kwa wafanyakazi wasiowajibika kunufaika na matokeo ya wenzao wanaofanya kazi kwa bidii.
“Itoshe kusema haitakuwa rahisi tena kwa wafanyakazi wasiowajibika kunufaika na posho zinazotokana na juhudi za wenzao. Kila mmoja atalazimika kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato chake,” alisisitiza.
Aidha Dkt. Kisenge aliwataka wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuweka mfumo madhubuti utakaomwezesha kila mfanyakazi kuona kwa uwazi utendaji wake pamoja na kipato anachostahili kulingana na mchango wake.
Akiwasilisha taarifa ya matumizi na makadirio ya bajeti ya taasisi hiyo, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa JKCI, CPA. Agnes Kuhenga taasisi hiyo itaendelea kulipia gharama za mafunzo kwa wafanyakazi watakaohitaji kuongeza elimu.
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi wote kwa juhudi zenu zilizowezesha kufikia mafanikio ya taasisi hii. Tumeweza kuboresha miundombinu na kuwajengea uwezo wafanyakazi 59 kutoka 54 wa mwaka uliopita ili kuboresha utendaji wao wa kazi”, alisema CPA. Agnes.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha kliniki mbalimbali katika maeneo tofauti nchini.
“Tumeanzisha kliniki tatu jijini Dar es Salaam ambazo ni Oysterbay, Kawe na Kariakoo ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi. Pia mkoani Arusha tumekabidhiwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ili kupunguza rufaa za wagonjwa wanaokuja Dar es Salaam kupata huduma”, alisema CPA. Agnes.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa chama hicho Hery Mkunda, aliipongeza JKCI kwa kuendelea kuweka mikakati ya kuiboresha taasisi pamoja na kuwajali wafanyakazi wake.
Mkunda alisema mkakati wa kuwalipa wafanyakazi kulingana na uzalishaji wao utaongeza ari ya kazi, uwajibikaji na ushindani wa kiutendaji ndani ya taasisi hiyo.
“Naunga mkono mkakati huu mpya wa kuwalipa wafanyakazi kulingana na uzalishaji wao kwani utaongeza ari na uwajibikaji kazini. Pia ni muhimu kuanzisha utamaduni wa kuchangia asilimia ndogo ya kipato cha mfanyakazi kwaajili ya maendeleo ya taasisi”, alisema Mkunda.
Aliongeza kuwa JKCI sasa imeendelea kujijengea sifa kama taasisi bora ya matibabu ya moyo nchini nan je ya nchi hali inayochochea ukuaji wa utalii tiba na kuongeza mapato ya taifa.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la JKCI, Adamu Sembe alisema kikao hicho ni muhimu katika kuwakumbusha wafanyakazi umuhimu wa kujituma, kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“Kikao hiki kinalenga kuwakumbusha wafanyakazi umuhimu wa kujituma na kuzingatia maadili ya kazi, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa na maslahi mapana ya taifa”, alisema Sembe.