Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

JKCI, Israel waimarisha huduma za upasuaji wa Moyo kwa watoto 252

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Monday, Apr 27, 2026
image description

Jumla ya watoto 252 wamepata huduma za upasuaji wa moyo kupitia ushirikiano uliopo kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na   Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel  hatua iliyosaidia kuokoa maisha yao.

Kati ya watoto hao 170 walifanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu zilizofanywa hapa nchini na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa SACH  huku watoto 82 wakipelekwa nchini Israel kwa matibabu zaidi.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI, Dkt. Naizihijwa Majani alipokuwa akizungumza na Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Gideon Behar alipotembelea taasisi hiyo kujionea huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na serikali ya Tanzania katika matibabu ya moyo.

Ziara hiyo ya Mhe. Balozi mpya wa Israel nchini Tanzania katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  iliyopo jijini Dar es Salaam ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya afya.

Dkt. Naizihijwa ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto  alisema tangu kuanza kwa ushirikiano huo  Israel imekuwa ikiunga mkono juhudi za JKCI katika kuboresha huduma za moyo kwa watoto.

“Tumefanya mambo makubwa kwa pamoja ikiwemo wataalamu wetu 15 kupata mafunzo nchini Israel  jambo ambalo limesaidia kuongeza idadi ya watoto wanaopata matibabu hapa nchini na kupunguza rufaa za kwenda kutibiwa  nje ya nchi”,  alisema Dkt. Naizihijwa.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo umevuka mipaka ya Tanzania kwa kuhusisha pia nchi jirani za Zambia, Kenya, Rwanda na Uganda jambo lililoongeza tija katika utoaji wa huduma na kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi barani Afrika.

Dkt. Naizihijwa alisema kupitia ushirikiano na SACH, JKCI pia inaisimamia hospitali ya moyo ya Zambia kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto, kutoa mafunzo kwa wataalamu pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za afya.

Kwa upande wake Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Behar alisema mahusiano ya muda mrefu kati ya JKCI na Israel yamekuwa na manufaa makubwa  hususan kupitia Shirika la Save a Child’s Heart (SACH)  ambalo limechangia kuokoa maisha ya watoto wengi wenye matatizo ya moyo.

Mhe.Balozi Behar alisema mahusiano kati ya Israel na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni mfano wa kuigwa katika ushirikiano wa kimataifa wenye lengo la kuokoa maisha ya watu hususan watoto.

Alisisitiza kuwa ushirikiano huo umejengwa katika msingi wa kuaminiana, kubadilishana ujuzi na teknolojia ya kisasa ya tiba ya moyo na kwamba Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha watoto wengi zaidi wanaozaliwa na matatizo ya moyo wanapata matibabu bora kwa wakati.

 “JKCI mnafanya kazi nzuri. Nimepita katika maeneo mbalimbali na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanyika, niko tayari kuendeleza ushirikiano huu wa kihistoria ili kuhakikisha watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo wanapatiwa matibabu kwa ufanisi. Kwa Kiyahudi tunasema, ukiokoa maisha ya mtoto mmoja umeokoa maisha ya dunia nzima”,  alisema Mhe. Balozi Behar.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Moyo kwa watoto wa JKCI ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto  Dkt. Godwin Sharau alisema ushirikiano huo umeleta mafanikio makubwa katika tiba ya moyo kwa watoto si Tanzania pekee bali pia katika ukanda wa Afrika.

Dkt. Godwin  alisema madaktari wengi pamoja na wauguzi wanaofanya  upasuaji wa moyo kwa watoto katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepata mafunzo yao nchini Israel kupitia ushirikiano na Shirika la Save a Child’s Heart (SACH).

Alieleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kitaalamu na kuwapa ujuzi wa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na mbinu bora za matibabu ya moyo kwa watoto jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma zinazotolewa nchini na kuongeza uwezo wa kufanya upasuaji wenye mafanikio makubwa hapa nyumbani.

“Ujuzi tulioupata nchini Israel umetuwezesha kutoa huduma bora hapa nyumbani na kusaidia nchi jirani zinazoanzisha vitengo vya matibabu ya moyo kwa watoto kufikia ufanisi wa juu. Kwa ufupi sisi ni mbegu iliyotoka Israel na kuja kupandwa Afrika”,  alisema Dkt. Sharau.

Akiwa katika Taasisi hiyo Mhe. Balozi Behar alitembelea maeneo mbalimbali ikiwemo vyumba vya upasuaji, wodi za wagonjwa, kliniki za wagonjwa pamoja na maabara ya kisasa inayotumia mfumo wa roboti kupima sampuli mbalimbali zikiwemo za damu ambapo alijionea kwa karibu namna huduma za kibingwa na kibobezi za moyo zinavyotolewa kwa ufanisi mkubwa na teknolojia ya kisasa.