Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Afya kwanza! JKCI Dar Group yawafikia watu 527 Kijichi

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Tuesday, Mar 17, 2026
image description

Watu 527 wamenufaika na huduma za uchunguzi wa afya katika kambi maalumu ya siku tatu iliyofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group kwa wakati wa Kijichi na maeneo jirani wilayani Temeke.

Kambi hiyo ilihusisha vipimo mbalimbali vya afya vikiwemo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo, shinikizo la damu,  kiwango cha sukari kwenye damu, macho pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya kinywa.

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema mwitikio wa wananchi umeonyesha haja kubwa ya Taasisi kuendelea kuwafuata wananchi mahali walipo.

“Katika kambi hii watu 224 tumewapa rufaa ya kufika katika Hospitali yetu ya Dar Group kwa ajili ya uchunguzi zaidi  wa huduma za upimaji tulizokuwa tunazitoa hapa kwani tumekutana na changamoto wa wagonjwa wanaoomwa lakini lakini hawaendi hospitali kupata huduma, za matibabu”,  alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktarin bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba alisema katika kambi hiyo watu 92 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na watu 118 walifanyiwa kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo.

“Baada ya kumalizika kwa kambi hii siku ya jumatano tutafanya na kambi nyingine ya uchunguzi wa afya katika kliniki yetu mpya iliyopo katika Soko Kuu la Kariakoo ghorofa ya tano, ninawaomba kwa wananchi mje kuchunguza afya zenu kwani huduma hii itatolewa bila malipo yoyote yale”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Kinywa na Meno wa JKCI Dar Group alisema  kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wananchi kutozingatia usafi wa kinywa na meno  jambo linaweza kusababisha maambukizi yanayoathiri moyo.

“Moyo unaweza kupata matatizo endapo usafi wa kinywa na meno hautazingatiwa. Virusi au bakteria kutoka kinywani vinaweza kuingia kwenye mfumo wa damu na kushambulia moyo”,  alisema Dkt. Mvungi.

Aliwahimiza wananchi kusafisha kinywa mara mbili kwa siku, asubuhi  baada ya kifungua kinywa na usiku baada ya kula chakula  ili kuzuia bakteria na virusi  vinavyoweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo ya moyo.

Mmoja wa wananchi waliopata  huduma katika kambi hiyo Steven Mtambo mkazi wa Mbagala Kizuiani, aliipongeza JKCI Dar Group kwa kampeni za uchunguzi wa afya zinazowawezesha watu kutambua hali zao mapema hasa vijana ambao mara nyingi hushughulikia afya zao pale changamoto za kiafya zinapojitokeza.

Kambi hiyo ya siku tatu, iliyohusisha wakazi wa Kijichi na maeneo jirani ya wilaya ya Temeke, ilizingatia kauli mbiu ya kampeni isemayo “Jua Namba Zako”, inayowaelekeza wananchi kufahamu shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, urefu, uzito na mafuta mwilini ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo