Huduma za Moyo zawafikia wananchi Njombe, DC atoa ombi Maalumu
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, Apr 27, 2026
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wameombwa kuendelea kufika katika Mkoa wa Njombe kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kutokana na ongezeko la uhitaji wa huduma hizo mkoani humo.
Ombi hilo limetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Juma Sweda, alipotembelea banda la JKCI katika Maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema ili kujionea huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa mbalimbali zinazotolewa katika banda hilo.
Mhe. Sweda alisema wananchi wa Njombe wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za moyo hivyo basi uwepo wa wataalamu hao kupitia maonesho hayo umeleta nafuu kubwa na kuongeza uelewa kuhusu magonjwa ya moyo na yasiyoambukiza.
“Wakazi wa Njombe msisite kutumia fursa hii kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwani yamekuwa tishio kubwa katika jamii yetu”, alisema Mhe. Sweda.
“Tunawashukuru sana wataalamu wa JKCI kwa kufikisha huduma hizi adhimu katika mkoa wetu. Tunaomba baada ya maonesho haya mpange tena kufika Njombe kutoa huduma zaidi ili kuwafikia wananchi wengi wenye uhitaji wa huduma hizo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma katika banda la JKCI waliishukuru serikali kwa kuruhusu kufanyika kwa maonesho hayo ambayo yamewapa fursa ya kuchunguza afya zao bila malipo karibu na maeneo yao.
Emanuel Elius, mkazi wa Njombe alisema amefaidika na huduma za uchunguzi wa moyo aliyoipa kwani hiyo ni mara yake ya kwanza kufanya vipimo vya moyo na kupata elimu muhimu kuhusu afya yake.
“Nilikuwa nikitumia sigara kwa muda wa miaka sita lakini leo nimepima moyo na kushauriwa kuacha uvutaji wa sigara ili kujikinga na matatizo ya moyo ikiwemo kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo”, alisema Emanuel.
Naye Rose Mvile mkazi wa Njombe alisema ameridhishwa na huduma alizopata, kutokana na ukarimu wa wataalamu wa JKCIna amepata fursa ya kuhudumiwa na madaktari bingwa bila gharama yoyote ile.
“Wanawake tuna majukumu mengi katika familia hivyo tunapaswa kutumia fursa hizi kuchunguza afya zetu mapema ili kulinda familia zetu pia ukifika katika banda la JKCI utapata elimu ya lishe bora ambayo itakusaidia kufahamu ”, alisema Rose.
Huduma za upimaji zinazotolewa katika kambi ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mkoani Njombe ni pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya moyo, kipimo cha shinikizo la damu (presha), kipimo cha sukari kwenye damu, kipimo cha mafuta mwilini, uwiano baina ya uzito na urefu (BMI), vipimo vya mfumo wa umeme wa moyo na jinsi moyo unavyofanya kazi na elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.