JKCI yapokea milioni 100 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Aug 07, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea msaada wa shilingi milioni 100 kutoka kwa kampuni ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa ajili ya kusaidia watoto wadogo wenye matatizo ya moyo wanaohitaji kufanyiwa upasuaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema msaada huo umeletwa katika wakati muafaka ambapo watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo hawana uwezo wa kifedha.
Dkt. Kisenge amesema kuwa msaada huo utarudisha matumaini kwa watoto na watanzania walikuwa wanashindwa kulipa gharama za matibabu ya moyo.
“Leo tumepokea msaada wa shilingi milioni 100 kutoka kwa wenzetu wa EACOP ambao utagharamia upasuaji wa watoto wadogo wenye matatizo ya moyo.”
“Huu ni msaada mkubwa unaobeba matumaini makubwa kwa familia zisizo na uwezo.” Amesema Dkt. Kisenge.
Ameongeza kuwa fedha hizo si tu kwamba zitasaidia watoto walio na hali mbaya bali pia zitaongeza uwezo wa taasisi katika kutoa huduma bora na endelevu kwa watoto wenye matatizo ya moyo.
“Kwa kuwa upasuaji wa moyo unagharimu fedha nyingi kwa mtoto mmoja ni wazi familia nyingi haziwezi kumudu kwa hiyo msaada huu utasaidia kurudisha maisha ya watoto waliokuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha lakini pia tutanunua vifaa muhimu vitakavyotumika kwenye upasuaji wa watoto.” Aliongeza Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa EACOP Tawi la Tanzania Geofrey Mponda amesema kwamba licha ya wao kujihusisha na mradi wa bomba la mafuta wameamua kujihusisha na masuala ya afya kama sehemu ya kuikumbuka jamii.
“Ingawa jukumu letu ni ujenzi wa bomba la mafuta tuliona ni muhimu kugusa maisha ya watu moja kwa moja watoto ni kundi nyeti na linapoguswa linagusa pia msingi wa taifa la kesho.”
“Watoto wanapozaliwa hawajui lolote kuhusu dunia hii wanapokumbwa na changamoto ya kiafya jamii inapaswa kuwasaidia kwa kuwaponyesha watoto hawa tunawaandaa kuwa viongozi na wataalamu wa baadaye.” Alisema Mponda.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani amesema kuwa takribani asilimia 80 ya watoto wamezaliwa na matatizo ya moyo.
“Karibu asilimia 80 ya watoto wanaopatiwa huduma hapa huwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo hata hivyo wakipatiwa matibabu mapema wengi wao hupata nafuu kabisa na huishi maisha ya kawaida.”
“Tangu tuanze kutoa matibabu haya tumeona mabadiliko makubwa wapo waliorejea shuleni wengine wako vyuoni na baadhi yao wanataka kuwa madaktari kama sisi, msaada huu unabadilisha maisha ya mtoto kwa ujumla.” Alisema Dkt. Majani.
Kupitia msaada huo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete itaweza kununua vifaa tiba kwaajili ya kuwasaidia watoto wenye shida ya moyo.