Wagonjwa 10 wenye matatizo ya mapigo ya moyo watibiwa JKCI
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Aug 06, 2025
Wagonjwa 10 wenye matatizo ya mapigo ya moyo yajulikanayo kitaalamu kama heart rhythm disorders wamefanyiwa upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo wakati wa kambi maalumu iliyofanyika kwa siku tano.
Kambi hiyo maalumu imefanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Africa la nchini Marekani na kumalizika hivi karibuni
Lengo la kambi hiyo lilikuwa kuwasaidia wagonjwa pamoja na kuimarisha ujuzi kwa madaktari wa JKCI na kuwapa nafasi wanafunzi wa shahada ya udaktari wakipata fursa ya kujifunza kwa vitendo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye alisema wagonjwa waliopatiwa matibabu katika kambi hiyo ni wale wenye matatizo katika mfumo wa utengenezaji wa mapigo ya moyo hali inayosababisha moyo kwenda kasi kupita kawaida, kuzimia na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha.
“Kwa wakati huu tulikuwa tumeandaa wagonjwa zaidi ya kumi wenye hitilafu katika mfumo wa mapigo ya moyo ili waweze kufanyiwa upasuaji katika kambi hii, tatizo la mfumo wa mapigo ya moyo husababisha moyo kwenda kasi sana na unaweza kupelekea kifo cha ghafla”, alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alieleza kuwa wagonjwa wengi hawakuwa na uwezo wa kifedha kuweza kulipia gharama za matibabu yao lakini JKCI kwa kushirikiana na Madaktari Africa walitoa huduma hizo kwa wagonjwa hao bila kujali hali yao ya kifedha.
“Karibu asilimia hamsini ya wagonjwa waliotibiwa safari hii hawakuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu lakini walipata huduma kupitia msaada wa Taasisi yetu na wa Madaktari Africa”, aliongeza. Dkt. Gandye.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Shirika la Madaktari Africa la nchini Marekani Matthew Sackett alieleza kuwa Madaktari Africa wanapenda kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo ili kwa pamoja waweze kushirikiana na wataalamu wa JKCI katika kuokoa maisha na kuendeleza ujuzi wa ndani kwa wataalamu wa JKCI.
“Tumekuja na timu yetu kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na kutoa mafunzo ya kina kwa wataalamu wa JKCI kuhusu matibabu ya magonjwa ya mapigo ya moyo, Ushirikiano wetu na wataalamu wa Taasisi hii ni wa kipekee,” alisema Dkt. Sackett.
“Matumaini yetu ni kuona huduma hizi za kitaalamu zikiendelea kutolewa hapa nchini kwa kutumia wataalamu wazawa waliopata ujuzi kupitia ushirikiano huo”, alisema Dkt. Sackett
Sackett alisema Madaktari Africa wanapenda kuona timu ya ndani ya wataalamu wabobezi wa moyo wanao uwezo wa kujitegemea na kutoa huduma zote za matibabu ya moyo.
JKCI itaendelea kushirikiana na mashirika ya ndani na ya kimataifa ili kuboresha huduma za afya ya moyo nchini Tanzania kwa kutumia wataalamu waliopatiwa mafunzo ya hali ya juu.