Elimu ya Lishe bora yatolewa katika maonesho ya Nanenane Dodoma
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Aug 06, 2025
Wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani wafaidika na elimu ya lishe bora inayotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maonesho ya 32 ya Kitaifa ya Nanenane
Elimu hiyo imejikita kuwasaidia wananchi kubadili mtindo wa maisha utakaowasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo yanaoongoza kwa vifo vingi duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Afisa Lishe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo alisema huduma ya lishe ni sehemu muhimu ya matibabu kwa watu mwenye magonjwa ya moyo, watu wenye uzito mkubwa na watu wenye tatizo la shinikizo la damu.
Lingindo alisema jamii pia inatakiwa kuacha matumizi ya sigara na unywaji wa pombe uliokithiri kwani kwa kutumia vilevi hivyo pia wapo katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Katika maonesho haya ya Nanenane hadi leo tumeweza kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi 70 ambapo kati yao wapo tuliowakuta na uzito mkubwa, shinikizo la damu na wengine wanaotumia vilevi kupindukia, kama watafuata ushauri wetu watakuwa salama”, alisema Lingindo.
Kwa upande wake mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo Rehema Msemwa alisema elimu aliyopata kuhusu lishe itamsaidia kupunguza uzito wake ili aweze kuulinda moyo wake usipate madhara yanayoweza kusababishwa na uzito mkubwa na mafuta mengi mwilini.
“Nimekuwa nikila chakula bila kuzingatia mlo kamili na muda sahihi wa kupata chakula hivyo kunipelekea kupata uzito mkubwa, baada ya kupata elimu hii ninaenda kuzingatia mlo kamili na kuongeza ulaji wa mbogamboga na matunda katika chakula changu”. alisema Rehema.
Naye Hassani Magesa mkazi wa Dodoma aliishauri JKCI kutoa elimu ya lishe bora wananchi kupitia vipindi vya Redio na Televisheni ili waweze kuisaidia jamii kuwa na afya bora itakayowasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Nimeshauriwa katika sahani yangu ya chakula nihakikishe nakula mbogamboga nyingi, matunda, vyakula vyenye protini na wanga kiasi huku nikiepuka kula vyakula vyenye mafuta mengi, lakini pia nimehaswa kufanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kwa siku mwili wangu uweze kukaa katika hali ya afya nzuri”, alisema Magesa