• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Tanzania mshindi wa pili maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara Zambia

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Tuesday, Aug 05, 2025
image description

Tanzania imeibuka mshindi wa pili kati ya nchi 25 zilizoshiriki katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yaliyomalizika jana jijini Lusaka.

Tanzania imeshika nafasi hiyo katika kundi la washiriki wa kimataifa ambapo mshindi wa kwanza ni Zimbabwe.

Akizungumza mara baada ya kupokea cheti cha ushindi Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule alishukuru kwa ushindi huo na kuahidi kuendelea kutangaza huduma mbalimbali zinazopatikana nchini kwa kila maonesho watakayoshiriki.

Mhe. Balozi Luteni Generali Mathew Edward Mkingule alisema ushindi huo ni matunda ya kazi kubwa iliyofanya na ubalozi wa Tanzania nchini Zambia pamoja na Taasisi zilizoshiriki maonesho hayo ambazo kwa pamoja zimepeperusha vyema bendera ya Tanzania.

“Katika banda la Tanzania tulikuwa tunatangaza huduma za matibabu ya kibingwa, huduma za usafirishaji na bidhaa mbalimbali zinazopatikana nchini zikiwemo kahawa, majani ya chai, korosho, juisi, pombe na vinginevyo. Pia tumetoa elimu na ushauri wa magonjwa mbalimbali”.
 

“Ni heshima kubwa kwa nchi yetu kupata cheti cha ushindi wa pili ambacho ni ishara ya ushirikiano madhubuti uliopo baina ya nchi zetu mbili za Tanzania na Zambia pia ni kutambua kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Taasisi zetu ambazo zimeshiriki katika maonesho haya”, alisema Mhe. Balozi Luteni Generali Mathew Edward Mkingule.

Mhe. Balozi Luteni Generali Mathew Edward Mkingule Serikali ya Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na ndiyo maana wananchi wengi wa Zambia na nchi jirani walifika katika banda hilo kwa ajili ya kufahamu huduma za matibabu ya kibingwa zinazopatikana nchini na kuona namna ambavyo watazipata huduma hizo.

Taasisi zilizoshiriki katika maonesho hayo na kutoa huduma a afya na usafirishaji katika banda la Tanzania ni  Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili  (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).