Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Wananchi wahimizwa kuzingatia lishe bora kujikinga na magonjwa ya moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Jul 08, 2026
image description

Vyakula vyenye mafuta mengi, sukari, chumvi kupita kiasi pamoja na vyakula vya wanga kwa wingi vyatajwa kuwa miongoni mwa vichocheo vya magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza iwapo mtu atavitumia kwa wingi.

Hayo yamesemwa na Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo alipokuwa akitoa elimu ya lishe kwa wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA).

Lingindo alisema lishe bora ni nguzo muhimu katika kuzuia magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo na kubainisha kuwa watu wengi hupata changamoto za kiafya kutokana na ulaji usiofaa, kutokufanya mazoezi ya mwili na kutumia vilevi kwa wingi.

 “Ni muhimu jamii ikabadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia lishe bora ili iweze kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanaathiri idadi kubwa ya watu na kupunguza nguvu kazi ya Taifa”, alisema Lingindo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea banda la JKCI walishukuru kwa kupata elimu muhimu ya lishe ambayo itawasaidia kubadili mtindo wa maisha na kulinda afya ya mioyo yao.

Fredy Kangi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema elimu ya lishe aliyoipata katika banda hilo ni ya faida kwake na familia yake kwani ataitumia kuhakikisha familia yake inajikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo. 

“Nimefurahi sana baada ya kupata elimu kuhusu lishe bora, nimefanya vipimo vyote vinavyotolewa katika banda hili, majibu yametoka vizuri na nimepewa ushauri wa kutosha kutoka kwa wataalamu ili niendelee kuwa na afya bora”, alisema Kangi.

Kangi alisema kabla ya kupata elimu kuhusu magonjwa ya moyo na lishe bora hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa ya moyo na madhara yake lakini kupitia maonesho ya SABASABA ameweza kukutana na wataalamu wa JKCI ambao wamempa elimu ya kutosha kuhusu magonjwa ya moyo na lishe bora.

“Kwa sasa nina amani na furaha kwa sababu najua hali yangu ya afya, nimepata mwongozo bora wa namna ya kuendelea kuitunza afya yangu na familia yangu”, alisema Kangi.