Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

JKCI na BMH kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo kutoka nchini Burundi

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Tuesday, Jul 07, 2026
image description

Watoto watano kutoka nchini Burundi wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kufanyiwa upasuaji wa moyo na wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).

Upasuaji huo kufanyika baada ya watoto hao kufanyiwa uchunguzi wa afya na kujadiliwa na jopo la wataalamu katika kambi maalumu ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa Watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema kambi hiyo imelenga kuwapatia matibabu ya kibingwa watoto hao na kuwapa  nafasi ya kuishi bila ya kuwa na maumivu.

Dkt. Sharau alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa kati ya watoto sita waliotakiwa kufanyiwa upasuaji huo mtoto mmoja hatofanyiwa upasuaji kutokana na hali yake ya kiafya  kuwa dhaifu hivyo kuendelea na matibabu mengine hadi hali yake itakapokuwa sawa.

“Tumewapokea watoto sita kutoka nchini Burundi lakini baada ya uchunguzi wa kina imeonekana mtoto mmoja hatutaweza kufanyiwa upasuaji wa moyo kwa kipindi hiki kutokana na hali yake ya kiafya, Leo tumewafanyia upasuaji watoto wawili, mmoja alikuwa na tundu katika vyumba vya juu vya moyo na mwingine mshipa wake wa damu uliopaswa kufunga baada ya kuzaliwa ulikuwa  haujafunga”, alisema Dkt. Godwin

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) John Meda alisema ushirikiano kati ya wataalamu wa Hospitali ya BMH na wenzao wa JKCI utaboresha huduma na kutoa ujuzi kwa wataalamu hao.

“Tunaamini baada ya kambi hii wataalamu wetu watabaki na ujuzi ambao utasaidia hapo baadaye katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Meda.

Naye Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Rehema Yona alisema watoto wote wamefanyiwa uchunguzi wa afya wa kina ili kuwawezesha wataalamu kubaini matatizo waliyonayo watoto hao na kujiridhisha kabla ya kuwafanyia upasuaji wa moyo.