Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Mkutano wa CardioTan 2026 wahitimishwa, wataalamu wapata ujuzi uchunguzi vipimo vya moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Sunday, Jun 07, 2026
image description

Mkutano wa nne wa kimataifa wa magonjwa ya moyo – CardioTan Imaging 2026 wafungua njia kwa wataalamu wa afya kuhakikisha magonjwa ya moyo yanaendelea kupatiwa ufumbuzi na kuongeza ujuzi wa wanataaluma wa vipimo vya moyo kwa kutumia kipimo cha Echocardiography.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mkutano huo jana jijini Dar es Salaam Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule alisema kupitia mkutano huu wataalamu wameweza kujadili visababishi vya magonjwa ya moyo, mikakati na namna ya kujipanga ili waweze kuongeza juhudi katika tafiti za magonjwa hayo na kuimarisha huduma zaidi. 

“Tunafahamu wote kuwa magonjwa ya moyo yamekuwa na madhara mengi ikiwemo kupata matibabu kwa muda mrefu hivyo kuleta gharama kubwa, lakini pia husababisha vifo vingi katika jamii zetu”, alisema Mhe. Mtambale

Mhe. Mtambale alisema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwa na maono mazuri kwa kuwekeza katika sekta ya afya hasa upande wa magonjwa yanayohitaji utaalamu wa kibingwa.

“Kutanuka kwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kunasaidia watu wengi kupata huduma hizo kwa urahisi katika maeneo yao, tunaishukuru JKCI kwa utayari wa wataalamu, juhudi na moyo mkubwa wa kiuzalendo katika kuwatibu watanzania na kuongeza ufahamu wa magonjwa hayo katika jamii”, alisema Mhe. Mtambale

Mhe. Mtambale alisema tatizo kubwa lililopo Tanzania kwa sasa sio wataalamu wala vifaa tiba bali kutokana na utafiti wa mwaka 2023 inaonesha kuwa mienendo ya maisha katika jamii imekuwa ni kichocheo kikubwa cha kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema mkutano huo umejikita katika upimaji wa magonjwa ya moyo kutokana na umuhimu wa kuyatambua magonjwa hayo mapema ili matibabu yaweze kutolewa kwa wakati na kupata matokeo mazuri.

“Tunawapongeza wataalamu wote walioshiriki mkutano huu kwani tunaamini wamepata mambo mazuri yatakayoweza kuwasaidia kwenda kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa moyo”, alisema Dkt. Angela

Dkt. Angela alisema kupitia mkutano huo wameweza kupata vifaa vyenye intelijensia ya kisasa kuwawezesha wataalamu waliokuja kuweze kupata elimu na kujua namna ya kuvipata na kuvitumia vifaa hivyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa mkutano huo wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendesha mkutano huo nchini na kuwapa ujuzi ambao utawasaidia kuwatambua wagonjwa wa moyo mapema.

Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Dkt. Kandi Lusingu alisema mkutano huo ni wa muhimu kwani umeonesha nchi ya Tanzania ilivyoendelea katika matibabu ya moyo kutokana na uongozi mzuri wa Serikali ya awamu ya sita kuboresha huduma za afya katika hospitali mbalimbali nchini.

“Zamani ilikuwa ni lazima mgonjwa wa moyo kwenda nje ya nchi kupatiwa matibabu lakini kutokana na ujuzi wa wataalamu wetu huduma hizi zinapatikana hapa nchini, pongezi nyingi kwa JKCI kwa kuwa mstari wa mbele kutoa huduma za matibabu ya moyo, lakini pia kutukutanisha hapa kupata utaalamu wa kuchunguza magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kandi

Dkt. Kandi alisema kupitia mkutano huo wameweza kujifunza namna ya kufanya vipimo vya moyo kwa wagonjwa mapema hata kwa watoto wanaozaliwa lengo likiwa ni kugundua haraka na kutoa huduma kwa wakati.

Naye Daktari kutoka Hospitali ya Wilaya ya Tabora Tumaini Fumbuka alisema mkutano huo umekuwa chachu kwa watoa huduma wa hospitali za wilaya kuweza kubaini magonjwa ya moyo na kuwaelekeza wananchi wenye magonjwa hayo kwenda sehemu sahihi kupata huduma kwa wakati.

Dkt. Fumbuka alisema kupitia mkutano huo wameweza kuhamasishwa kuhusu upimaji wa picha sahihi, na ubainifu wa magonjwa ya moyo katika vituo vya afya na hospitali za wilaya kutokana na magonjwa hayo kukua kwa kasi.

Mkutano wa nne wa kimataifa wa magonjwa ya moyo – CardioTan Imaging 2026 wenye kauli mbiu “Uchunguzi mahiri kwa moyo imara” umewakutanisha wataalamu wa afya zaidi ya 600 kutoka nchi zaidi ya 16, pia kupitia mkutano huo Chama cha wataalamu wa kupima moyo kwa kutumia kipimo cha Echocardiography Tanzania (Echocardiograph society) kilizinduliwa.