Mkutano wa CardioTan Imaging 2026, WHO yaeleza maendeleo ya JKCI
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Sunday, Jun 07, 2026
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yatajwa kuwa moja ya taasisi za afya nchini yenye ubunifu na kuleta mafanikio katika sekta ya afya huku ikizidi kujijengea sifa katika Bara la Afrika.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Program Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Sisay Tegegne wakati akimuwakilisha Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, Shirika la Afya Duniani (WHO) Prof. Mohame Janabi kufungua mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026 unaofanyika katika ukumbi wa Blue Sapphire jijini Dar es Salaam.
Dkt. Tegegne alisema ni jambo la kufurahisha kuona mkutano huo muhimu unawakutanisha wataalamu wa afya kutoka nchi mbalimbali ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za uchunguzi, utambuzi wa haraka wa vipimo vya moyo na matibabu ya magonjwa hayo huku ukionesha maendeleo yanayopatikana katika sekta ya afya nchini Tanzania.
“Tanzania ipo katika nafasi nzuri katika huduma za matibabu ya moyo kutokana na historia yake ya maendeleo, upanuzi wa huduma umekuwa ukiendelea ndani na nje ya mipaka ya nchi jambo ambalo ni la kujivunia”, alisema Tegegne
Dkt. Tgegne alisema mustakabali wa huduma za matibabu ya moyo nchini una matumaini makubwa kutokana na kuongezeka kwa utaalamu, ubunifu na matumizi ya teknolojia mpya, pia huduma za upandikizaji wa moyo zinazotarajiwa kuanza kutolewa Tanzania baada ya miaka mitano zitaongeza maendeleo katika sekta ya afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kupitia mkutano huo JKCI imeweza kuwakutanisha wataalamu kutoka nchi mbalimbali duniani ili kwapamoja waweze kushirikiana na kubadilishana mawazo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo.
“Uwekezaji uliofanywa na Serikali yetu katika sekta ya afya ni mkubwa, hivyo tumetaka kuionesha dunia ni jinsi gani Tanzania imewekeza vya kutosha katika huduma za afya hasa upande wa matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema magonjwa ya moyo na yale yasiyoambukiza yanazidi kuongezeka na kuchangia vifo vya watu wengi ambapo jumla ya watu milioni 17 duniani hupoteza maisha kutokana na magonjwa hayo.
“Kwa hapa Tanzania magonjwa ya moyo yanafikia asilimia 25 kwa sasa, hivyo ni lazima tuwe na vifaa vya kugundua magonjwa haya ili tuweze kuwatibu vizuri wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Kisenge
Wakielezea mafanikio ya mkutano huo washiriki wa mkutano walisema Tanzania ipo katika mwelekeo sahihi wa kuwa kinara wa huduma za matibabu ya moyo si tu ndani ya nchi bali pia kusini mwa jangwa la Sahara.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mwanzilishi wa huduma za moyo Tanzania Johnson Rwakatare alisema huduma walizoanzisha kipindi hicho na mafanikio yaliyopo sasa yanawatia moyo waanzilishi wa huduma hizo nchini.
“Nakumbuka wakati tunaanza huduma za matibabu ya moyo hapa nchini tulikuwa watatu lakini sasa hivi wataalamu wa magonjwa ya moyo ni wengi na wameweza kuendeleza huduma hizi kwa kujifunza mbinu mbalimbali za kuyatibu magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Rwakatare
Dkt. Rwakatare alisema baada ya Serikali kuonesha dhamira kubwa ya kuinua huduma za matibabu ya moyo nchini, huduma hizo zimeboreshwa na kuifanya Tanzania kujivunia kuwa kinara wa matibabu ya moyo ikilinganishwa na nchi zilizoendelea.
Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026 wenye kauli mbiu uchunguzi mahiri kwa moyo imara unafanyika kwa siku tatu na kuwakutanisha wataalamu wa afya kutoka nchi za Chile, Kenya, Marekani, Uganda, Misri, na Afrika ya Kusini.