Kampeni ya “Jua Namba Zako” yawafikia Mashabiki wa Arsenal
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, May 30, 2026
Mashabiki wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Arsenal wapata elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na kuzijua namba zao za afya wakati wa hafla ya kusherehekea ushindi wa timu hiyo iliyofanyika leo katika viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo imefanyika sambamba na tukio la Ongea na Waziri wa Afya kutoa motisha kwa mashabiki hao kufanyiwa uchunguzi wa afya, kuhamasisha kampeni ya Jua Namba Zako na kuikumbusha jamii kuwa na mtindo bora wa maisha.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joyce Kyando alisema JKCI itaendelea kuihamasisha jamii kuzifahamu namba zao za afya na kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
“Tunaamini mashabiki hawa wa Arsenal wakishazijua namba zao kupitia hafla hii watajenga tabia ya kupima afya mara kwa mara na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”,
“Unaweza kumuona mtu anafanya mazoezi kila siku lakini bado akawa na mafuta mengi kwenye damu, hivyo tusiangalie muonekano wa nje tukajiona salama, tupende kufanya uchunguzi wa afya”, alisema Dkt. Joyce
Kwa upande wao mashabiki wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Arsenal walioshiriki hafla hiyo wameishukuru Wizara ya Afya kuiwezesha JKCI kufikisha huduma za uchunguzi wa afya kwa mashabiki hao.
Da hope shabiki wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Arsenal alisema wakati mashabiki wa timu hiyo wanapata burudani pia wamepata nafasi ya kufanya uchunguzi wa afya na ushauri kutoka kwa wataalamu mabingwa wa magonjwa ya moyo.
Naye Gideon Rwegelela shabiki wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Arsenal alisema kupitia hafla hiyo watanzania wengi wataelimika na kuzifahamu namba zao ambazo Wizara ya Afya imekuwa ikihimiza jamii kuzijua na kuchukua hatua.