Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Jamii yahimizwa kupima Afya mara kwa mara kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Saturday, Mar 14, 2026
image description

Jamii imetakiwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kufahamu namba zao za kiafya ili kujikinga na madhara yanayosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza. 

Rai hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu wakati wa uzinduzi wa kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi wa afya inayofanywa na wataalamu wa hospitali hiyo kwa wakazi wa Kijichi wilaya ya Temeke na maeneo ya jirani.

Dkt. Shemu alisema kambi hiyo imelenga kuwahamasisha wananchi kuchunguza afya zao mapema hususan magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la juu la damu, kisukari na magonjwa ya moyo ambayo kwa sasa yanaongezeka kwa kasi katika jamii hasa katika nchi zinazoendelea na zile zenye uchumi wa kati.

Alifafanua kuwa katika siku ya kwanza ya kambi hiyo wananchi 205 walipatiwa huduma mbalimbali za uchunguzi wa afya ikiwemo uchunguzi wa kinywa na meno, macho, uvimbe, ngiri, shinikizo la damu, sukari kwenye damu pamoja na vipimo maalumu vya moyo. Kati yao takribani watu 100 walipatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Dar Group  kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.

“Takwimu zinaonyesha magonjwa ya moyo hasa shinikizo la juu la damu yanaongezeka hata kwa vijana hali inayoweza kuathiri nguvu kazi ya taifa ikiwa hatua za mapema hazitachukuliwa” ,alisema Dkt. Shemu.

Kwa upande wao wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo waliwapongeza wataalamu wa JKCI Dar Group kwa kuwafikishia huduma wananchi wa Kijichi na maeneo ya jirani na kuwataka kuendelea kutoa huduma hizo mara kwa mara ili kusaidia jamii ambayo haifikirii kwenda hospitali kufanya uchunguzi wa afya hadi pale inapopatwa na changamoto za kiafya.

“Watu wengi hatuendi hospitali mpaka tuumwe sana. Leo nimefanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa nina tatizo la macho na kushauriwa nifike hospitali kwa matibabu zaidi. Nawapongeza sana JKCI kwa kutuletea huduma hizi karibu”, alisema Beatrice Kinyamasongo mkazi wa Mbaga Kuu.

Naye Gabriel John mkazi wa Kijichi alisema huduma za uchunguzi wa afya zinazotolewa kupitia kambi kama hizo ni muhimu kwa wananchi kwani zinawasaidia kujua hali zao za kiafya mapema.

“Tumefundishwa hapa umuhimu wa kujua namba zetu za shinikizo la damu, sukari kwenye damu pamoja na uwiano wa urefu na uzito. Hii itatusaidia kubadili mtindo wa maisha na kujikinga na magonjwa ya moyo”, alisema Gabriel.

Kambi hiyo ya uchunguzi wa afya kwa wakazi wa Kijichi ni sehemu ya juhudi za JKCI za kusogeza huduma za kibingwa bobezi karibu na wananchi pamoja na kuongeza uelewa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ili kuchochea hatua za kinga na matibabu mapema.