Siku ya Msikilizaji Habari Maalum Media yaleta uchunguzi wa Moyo bure Ngaramtoni
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Feb 21, 2026
Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na elimu ya afya kwa mamia ya wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Msikilizaji yaliyoandaliwa na Habari Maalum Media, yaliyofanyika Ngaramtoni mkoani Arusha.
Katika tukio hilo lililowakutanisha zaidi ya wasikilizaji 400 wa kituo hicho, wananchi walipata fursa ya kupima afya za mioyo yao, kupimwa viashiria mbalimbali vya hatari pamoja na kupewa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo, Matroni wa Wauguzi wa ALMC, Sr. Flora Kasembe alisema zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa limewafikia wananchi wengi ambao hawapati muda wa kufika hospitalini kwa uchunguzi wa afya.
Alisisitiza kuwa uchunguzi wa afya mara kwa mara ni muhimu katika kugundua matatizo ya kiafya mapema na kuanza matibabu kwa wakati hatua inayosaidia kupunguza madhara makubwa, gharama za matibabu na vifo vinavyoweza kuzuilika.
“Wananchi wengi hupata matatizo makubwa ya kiafya kwa kuchelewa kugundua magonjwa. Tunawahamasisha kujenga utaratibu wa kupima afya zenu mara kwa mara ili kuzuia madhara yanayoweza kuepukika”, alisema Sr. Flora.
Aidha Sr. Flora ambaye ni Afisa Muuguzi aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kambi maalumu za huduma za kibingwa zitakazofanyika bila malipo katika Hospitali ya ALMC, ikiwemo kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya mifupa na mishipa ya fahamu watakayoifanya kwa kushirikiana na wataalamu kutoa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) tarehe 23-27/02/2026.
"Kambi nyingine ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo tutaifanya tarehe 27-28/2/2026 kwa kushirikiana na wataalamu wenzetu kutoka Shirika la Heart to Heart Association for Sustainable Develepment la nchini Misri", alisema Sr. Flora.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma ya uchunguzi wa moyo walieleza kufurahishwa kwao na upatikanaji wa huduma za bure karibu na makazi yao huku wakisema imewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata ushauri wa kitaalamu bila gharama.
Ernest Mollel mkazi wa Ngaramtoni alisema huduma hiyo imekuwa ya manufaa makubwa kwa jamii kwani watu wengi hawana tabia ya kupima afya hadi wanapoumwa.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, upimaji wa mara kwa mara ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwani husaidia kugundua vihatarishi mapema na kuwezesha kupata tiba na kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha kabla hali haijawa mbaya.
Kupatikana kwa huduma hizo ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kinga na uchunguzi wa mapema.