Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

JKCI yahimiza kupima afya mapema: Fursa adimu kwa washiriki wa mkutano wa e-GA

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Friday, Feb 20, 2026
image description

Taasisi ya Moyo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watumishi wa umma walio hudhuria Kikao Kazi cha 6 cha Serikali Mtandao (e-GA) kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) kwa siku tatu.

Akizungumza wakati wa kambi hiyo daktari wa Taasaisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sahiya Yahya alisema taasisi hiyo imesogeza karibu huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watumishi wa umma kupitia kikao kazi cha e-GA jijini Arusha.

Dkt. Sahiya alisema huduma zinazotolewa ni pamoja na upimaji wa shinikizo la damu, kiwango cha sukari mwilini, kipimo cha kuangalia utendaji kazi wa moyo na ushauri kutoka kwa daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ili kubaini mapema changamoto za magonjwa ya moyo.

“Tupo Arusha kwenye mkutano wa e-GA hapa AICC ambapo tunatoa huduma za upimaji wa presha, kisukari, kuonana na Daktari Bingwa wa Moyo pamoja na kipimo cha kuangalia utendaji kazi wa moyo”. AlisemaD kt. Sahiya.

Dkt. Sahiya alisema katika uchunguzi uliofanyika baadhi ya wananchi wamebainika kuwa na shinikizo la juu la damu na wamepewa ushauri wa kitaalamu ili kujikinga na magonjwa ya moyo.

“Baadhi ya watu tuliowaona wana shinikizo la juu la damu tumewapa ushauri wa kubadilisha mtindo wa maisha na wengine tumewapa rufaa kuja Taasisi ya Moyo Jaksys Kikwete (JKCI) na kwenye tawi letu la Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC)”, alisema Dkt. Sahiya

Kwa upande wake Afisa Ununuzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) Baraka Mbaniku alisema kuwa ujio wa wataalamu hao umekuwa ni fursa kwa washiriki wa mkutano huo.

“Huduma hizi kwa kawaida ni ghali ukizifuata mwenyewe lakini hapa zinatolewa bure kabisa hivyo ni muhimu watu wafike kuangalia afya zao”, alisema Baraka.

Naye Mfanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Thomas Ngaka aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma hizo walizozitoa huku akisema zimekuwa msaada mkubwa kwake.

“Huduma ni za haraka na nashukuru Mungu afya yangu ya moyo iko vizuri hii ni fursa ambayo ingenigharimu muda na fedha kwenda hospitalini”, alisema Thomas.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuhimiza jamii kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili waweze kugundua na kujikinga na magonjwa mapema kabla hayajaleta madhara makubwa.