Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Watu 253 wafanyiwa uchunguzi wa afya mkutano wa e-GA

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Friday, Feb 20, 2026
image description

Watu 253 wakiwemo wanaume 140 na wanawake 113 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku tatu iliyofanyika wakati wa kikao kazi cha sita cha Serikali Mtandao (e-GA) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).

Katika kambi hiyo watu 49 walihitaji uchunguzi wa kitaalamu zaidi hivyo kupewa rufaa ambapo watu 28 walipewa rufaa kwenda JKCI, watu 13 walipewa rufaa kwenda Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) na watu nane walipewa rufaa kwenda hospitali nyingine kwa ajili ya matibabu zaidi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwasasa inasimamiwa na JKCI Dkt. Salehe Mwinchete alisema mwitikio wa washiriki wa kikao hicho umekuwa mkubwa ambao umetoa fursa kwa washiriki hao kuweza kupata taarifa sahihi zinazohusu magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo. 

“Washiriki wa mkutano huu wameweza kufanyiwa uchunguzi wa afya kwa kuwapima vipimo vya awali kuangalia viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, sukari kwenye damu, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ya moyo lengo likiwa kuwasaidia washiriki kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa ya moyo”, 

“Wapo watu tuliowakuta na matatizo ya mishipa ya damu ya moyo kuziba, mapigo ya moyo kutokuwa sawa pamoja na ugonjwa wa kisukari hali inayoashiria uwepo wa vihatarishi vya magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Salehe

Dkt. Salehe alisema kumekuwa na changamoto ya mwitikio mdogo wa vijana kujitokeza kufanya uchunguzi wa afya, lakini Taasisi hiyo imejipanga na kutengeneza mbinu za kuwafikia vijana kupitia mikutano na majukwaa ya kijamii.

Kwa upande wake Afisa TEHAMA wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Emina Mbele alisema kupitia kambi hiyo ameweza kufaidika na huduma zilizokuwa zinatolewa kwani ameweza kupima shinikizo la damu, sukari kwenye damu, uzito na kufanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO).

“Nawahamasisha watu wapime afya zao hata kama hawana dalili kwa sababu huduma hii imeletwa karibu nasi kupitia kikao chetu, tusiogope tujitokeze kwa wingi kuchunguza afya zetu”, alisema Emina.

Naye Afisa TEHAMA wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Geofrey Justine alisema ameridhishwa na mapokezi na huduma alizopata kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuishauri Taasisi hiyo kuendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi ili waweze kupungua idadi ya watu wanaopata magonjwa ya moyo.  

“Ninaomba huduma kama hizi zisiishie kwenye mikutano mikubwa tu, bali ziende hadi mikoani ambako watu wengi wana changamoto za afya ikiwemo magonjwa ya moyo”, alisema Geofrey

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikifanya kambi maalumu katika mikutano mbalimbali nchini ikiwa ni mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelewa, kuhamasisha uchunguzi wa afya mapema na kupunguza tatizo la magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.