Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Washiriki 600 kutoka mataifa 60 kukutana Dar kwa mkutano wa kimataifa wa moyo - CardioTan Imaging 2026

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Friday, Jan 23, 2026
image description

Zaidi ya washiriki 600 kutoka mataifa zaidi ya 60 duniani wanatarajiwa kushiriki katika Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026, unaoandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Heart Team Africa Foundation (HTAF) pamoja na Andalusia Group of Medical Services kutoka nchini Misri.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe  4 hadi 6 mwezi Juni 2026 katika Ukumbi wa Blue Sapphire, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, ukilenga kuwakutanisha wataalamu wa afya, watafiti na wadau wa sekta ya moyo kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kujadili maendeleo ya kisayansi na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kuutambulisha mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo akiliunde (Artificial Intelligence – AI) na mbinu bunifu za uchunguzi wa moyo.

“Mkutano wa CardioTan 2026 – CardioTan Imaging 2026, utakuwa fursa muhimu kwa wataalamu wa afya kupata ujuzi wa kisasa katika uchunguzi wa moyo na vipimo vya kitaalamu kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu,” alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa mkutano huo pia utakuwa na mchango mkubwa katika maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, kwa kuwa utaweka mkazo katika eneo la Sports Cardiology (Afya ya moyo katika michezo), jambo litakalowasaidia wataalamu wa afya kujiandaa kukabiliana na changamoto za kiafya kwa wanamichezo na jamii kwa ujumla.

“Kwa kuwaleta pamoja wataalamu wa ndani na wa kimataifa, tunajenga uwezo wa kitaifa wa kushughulikia changamoto za afya ya moyo kwa kutumia mbinu za kisasa,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa JKCI na Mwenyekiti wa Kamati ya Kisayansi ya mkutano huo, Dkt. Tatizo Waane alisema mkutano huo umejikita zaidi katika kuangazia umuhimu wa uchunguzi wa kina wa magonjwa ya moyo kwa kutumia teknolojia za kisasa.

“Ili mgonjwa apate tiba sahihi, lazima uchunguzi uwe wa kina na wa kitaalamu. Kupitia mkutano huu, tutajadili na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za kisasa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo,” alisema Dkt. Waane.

Naye Mjumbe wa Baraza la Mionzi Tanzania, Catherine Malika, akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Baraza hilo, aliwataka wataalamu wa afya nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo ili kuongeza ujuzi wao wa matumizi ya teknolojia za kisasa.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa tiba vya kisasa kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali. Mkutano huu ni fursa ya kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa ufanisi na weledi,” alisema Catherine.

Kwa upande wake  Mkuu wa Kitengo cha Vipimo vya Moyo wa JKCI na mwanzilishi wa Chama cha Vipimo vya Moyo Tanzania (TES), Dkt. Engarasiya Kifai, alisema mkutano huo utaongeza wigo wa maarifa kwa wataalamu wa ndani na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya kimataifa ya elimu ya afya ya moyo.

“Mataifa mengi yaliyoendelea barani Ulaya na Amerika yamepiga hatua kubwa kupitia mikutano ya kitaaluma kama hii. Kupitia CardioTan Imaging 2026, nasi tunaendelea kujifunza na kujenga uwezo kwa manufaa ya wagonjwa wetu,” alisema Dkt. Engarasiya.

Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo wa mwaka 2026 una kauli mbiu isemayo “Uchunguzi Mahiri wa Moyo, kwa Moyo Imara”.

Mkutano huo wa Kimataifa wa magonjwa ya moyo ni wa nne  tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023  na umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kitaaluma litakaloikutanisha dunia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maendeleo ya huduma za moyo.