JKCI na Watalaamu wa Ujerumani waokoa Maisha ya watoto 15
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Sunday, Mar 15, 2026
Watoto 15 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ikiwemo matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika mpangilio wake wa kawaida wamefanyiwa upasuaji katika kambi maalum ya siku tano iliyofanyika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo iliyomalizika jana ambao iliyoratibiwa na msanii wa muziki wa Bongo Fleva Ben Paul ilifanyika kwa kushirikisha wataalamu wa JKCI pamoja na wenzao kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Moyo Mission ya nchini Ujerumani.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema ushirikiano kati ya JKCI na Moyo Mission katika kutoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na uzoefu na uwezo walionao watalamu hao kutoka Ujerumani.
“Tunaishukuru serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuruhusu timu hii ya wataalamu wanne kutoka Ujerumani wakiwemo madaktari bingwa wawili wa upasuaji wa moyo, mtaalamu mmoja wa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) pamoja na mtaalamu mmoja wa mitambo ya mapafu kuja JKCI na kuongeza nguvu”, alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela alisema ushirikiano kati ya JKCI na Moyo Mission ni wa kwanza kufanyika ambapo pamoja na kutoa matibabu kwa watoto watalaamu hao pia wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kujifunza mbinu mbalimbali za kitabibu.
"Tunashukuru kwani watoto wa kitanzania wamenufaika na kambi hii lakini pia sisi kama JKCI tumefaidika kwa kupata vifaa tiba vya kisasa kwa gharama naafuu kutokana na washirika wetu kuwa karibu na kampuni zinazotengeneza vifaa vya matibabu ya magonjwa ya moyo", alisema Dkt. Angela.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo cha Heart Center kilichopo Hamburg Ujerumani ambaye pia ni Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto Dkt. Daniel Biermann alisema wamechagua kushirikiana na JKCI kutokana na Taasisi hiyo kuwa na miundo mbinu bora inayowawezesha kutoa huduma za kibingwa kwa ufanisi.
"Mazingira mazuri yamechangia kufanikisha upasuaji wa moyo kwa watoto na tunatarajia kuendeleza ushirikiano huu kwa muda mrefu na tunapanga kuja zaidi ya mara mbili kwa mwaka ili kuwasaidia watoto wa Kitanzania kupata matibabu na kuokoa maisha yao,"alisema Dkt. Biermann.
Naye Mratibu wa ushirikiano huo kutoka Ujerumani Marie Biermann alisema lengo la ushirikiano huo ni pamoja na kuwajengea uwezo watalaamu wa ndani kupitia mafunzo mbalimbali yatakayowasaidia kujiendeleza kitalaamu katika masuala ya matibabu ya magonjwa ya moyo.
"Taasisi hii ina wataalamu wenye uwezo mkubwa katika matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto hivyo kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo zaidi ili waendelee kutoa huduma za kibingwa na za kibobezi" alisema Marie.
Mmoja wa mzazi ambaye mtoto wake alifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu kwenye moyo katika kambi hiyo Nyaboke Korosso aliwashukuru watalaamu wa afya waliofanya upasuaji huo kwa mafanikio na kuokoa maisha ya mtoto wake.
“Namshukuru Mungu na madaktari wote waliofanikisha upasuaji wa mtoto wangu ambaye ameteseka na maumivu ya kifua upande wa kushoto kwa muda mrefu na sasa nina matumaini makubwa ya kuona akirejea katika hali yake ya kawaida”, alisema Nyaboke.
Kupitia kambi hiyo watoto hao wamapata huduma za kibingwa za upasuaji wa moyo hatua inayosaidia kurekebisha matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo na kuwapa nafasi ya kuishi maisha yenye afya bora.
-Mwisho-