Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Furaha ya watani wa jadi, uhakika wa Afya: Mashabiki wa Simba na Yanga kupimwa moyo bure

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Saturday, Dec 20, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo wakati wa mechi ya Simba na Yanga itakayofanyika siku ya Jumapili Disemba 21 mwaka huu.

Upimaji huo utakaotolewa bila gharama pia utafanyika kwa kila mwananchi atakayefika katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa KMC uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imeona ichukue jukumu la kufika katika Uwanja wa KMC wakati wa mechi hiyo kutoa huduma kwa wananchi kwani wengi wao hawana tabia ya kuchunguza afya mara kwa mara.

“Magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo yanaongezeka kwa kasi, tumechukua jukumu la kuwafuata mashabiki na wachezaji wa timu hizi kubwa ili tuweze kuwapima na kuwapa elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza” alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza wataalamu wa afya na vifaa tiba hivyo siku ya mechi hiyo JKCI itakuwa na vifaa vinavyotumia akili unde kuchunguza moyo unavyofanya kazi.

“Huduma hii imetolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mashabiki wa timu hizi ili wanapokuwa na furaha kushabikia timu zao basi wawe na uhakika wa afya zao”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake msemaji wa timu ya mpira wa miguu ya Simba Sports Club Ahmed Ally alisema mwanzoni wakati mechi hiyo ikiandaliwa ilikuwa na kusudi la watu kwenda kupata burudani lakini jambo hilo limeongezeka thamani na kutoa fursa kwa mashabiki wa timu hizo kupata huduma za afya.

Ahmed alisema kwa wale ambao wamepitia changamoto za kuugua ama kuuguza wanafahamu thamani ya kupata vipimo na matibabu kutoka kwa wataalamu mabigwa wabobezi, hivyo mashabiki hao watumie vizuri fursa hiyo adhimu ambayo imewafikia kirahisi.

“Kupitia mechi yetu ya Simba na Yanga tunaenda kapata vipimo na matibabu ya moyo kwa haraka, bila gharama zozote, nauli yako utakayotoka nayo nyumbani ndio itakuwezesha kufanya uchunguzi wa afya chini ya wataalamu bingwa kutoka JKCI”, alisema Ahmed

Naye msemaji wa timu ya mpira wa miguu ya Young Africans (YANGA) Ally Kamwe alisema mashabiki wa Yanga wameshukuru kwa fursa ambayo JKCI imeitoa kwao kwani mchezo kati ya timu hizo unahusisha hisia kubwa ambayo inaweza wasababishia mashabiki kupata magonjwa ya shinikizo la damu.

“Kwa nafasi yenu mmeamua kuitumia mechi hii ya mashabiki wa Yanga na Simba kutoa huduma za matibabu ya moyo bila gharama, tunawashukuru sana, mwanzoni tuliona ni mechi ya kawaida kumbe ni mechi ambayo inaenda kusaidia jamii yenye uhitaji wa uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Ally

 “Mashabiki wa Yanga tunapata raha lakini kucheki afya pia ni muhimu, kwani tunaweza kuwa tunapata raha Yanga lakini furaha hiyo inaweza kuharibiwa katika maeneo yetu mengine na kutusababishia shida za moyo, fursa hii tuitumie vizuri”, alisema Ally

Upimaji huo utakaonza kutolewa kukanzia saa mbili asubuhi siku ya Jumapili utahusisha wataalamu mabingwa wa magonjwa yasiyoambukiza na wataalamu wa lishe huku ukienda na Kauli mbiu isemayo “pima moyo wako leo uishi kesho, jitokeze kupima”,.