Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Ziara ya Kujifunza: Viongozi wa Congo wapata huduma za kibingwa za Moyo JKCI

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Friday, Feb 27, 2026
image description

Uwekezaji wa Tanzania katika sekta ya afya umeendelea kuvuka mipaka baada ya ujumbe wa viongozi 15 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ukiongozwa na Gavana wa Jimbo la Maniema kufanyiwa uchunguzi wa moyo na kuvutiwa na ubora wa huduma katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Ujumbe huo ulipatiwa huduma katika tawi la JKCI lililopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam kufuatia ziara yao ya kujifunza kuhusu mafanikio ya Tanzania katika huduma za afya bingwa na bobezi zikiwemo za matibabu ya moyo.

Akizungumza baada ya kufanyiwa uchunguzi huo Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Juma Mshana alisema ziara hiyo imelenga kuwaonesha viongozi hao namna Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyowekeza kwa kiwango kikubwa katika hospitali za umma.

Balozi huyo ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika nchi za Congo Brazzaville, Afrika ya Kati, Cameroon, Cab Bon na Equatorial Guinea alisema anakusudia mwezi ujao kuwaleta magavana kutoka majimbo ya Lualaba na Haut Katanga yaliyopo nchini DRC ili kujifunza jinsi ambavyo Tanzania imesonga mbele katika sekta ya afya.

Alibainisha kuwa mwezi ujao anatarajia kuwaleta magavana kutoka majimbo ya Lualaba na Haut Katanga kwa ziara kama hiyo ya kujifunza na kubadilishana uzoefu.

"Kwa niaba ya ujumbe wangu, tunamshukuru Dkt. Kisenge na menejimenti ya JKCI kwa mapokezi mazuri na kwa kutupatia huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo bila gharama. Huu ni ushahidi wa moyo wa kiungwana na ubora wa huduma zinazotolewa hapa", alisema Mhe. Balozi Mshana.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge alisema ujumbe huo umefurahishwa na uwekezaji wa Serikali katika hospitali za umma huku akibainisha kuwa katika DRC sekta binafsi ndiyo yenye mchango mkubwa zaidi katika huduma za afya.

"Tuna kila sababu ya kujivunia uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika huduma za afya, hususan huduma za kibingwa na kibobezi ambazo sasa zinavutia hata wageni kutoka nje ya nchi",  alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema ujumbe kutoka Congo umefurahia huduma za JKCI, mapokezi, vipimo walivyofanyiwa na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa kuelezea uwekezaji uliofanywa Tanzania katika sekta ya afya watakaporudi nchini kwao.

Naye Mshauri wa Masuala ya Biashara kutoka DRC, Dkt. George Oyema alisema licha ya kutembelea nchi nyingi ikiwemo Marekani, India na China amevutiwa na kiwango cha teknolojia na utaalamu aliouona JKCI.

"Nimeona mashine za kisasa na huduma zenye viwango vya juu kabisa matibabu ya moyo. Hii ni taasisi inayoweza kushindana kimataifa”.

“Tunawashukuru sana Taasisi hii inayojihusisha na matibabu ya moyo kwa kutupatia nafasi ya kuangalia afya zetu tumefurahi sana, watu hawa wana upendo wa aina yake”, alisema Dkt. Oyema

Ziara hiyo imeongeza sura ya Tanzania kama kitovu cha huduma za afya za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kuimarika katika nyanja za afya na uwekezaji.

  • Mwisho -