Kambi Maalum ya Upimaji na Matibabu ya Moyo Yawafikia watu 302 Arusha
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, Mar 02, 2026
Watu 302 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku mbili iliyofanywa na wataalamu wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre ambayo kwa sasa inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Heart to Heart Association for Sustainable Development na Egyptian African Heart Association (EAHA) za nchini Misri.
Akizungumza wakati wa kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Eva Wakuganda alisema kati ya wagonjwa hao watoto 18 waligundulika kuwa na magonjwa mbalimbali ya moyo, huku watu wazima 235 wakiwemo wanawake 112 na wanaume 121 miongoni mwao wamegundulika kuwa na shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka, hitilafu za umeme wa moyo na kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo.
Dkt. Eva alisema kuwa lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kubaini mapema wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.
“Tumewapa wagonjwa rufaa kwa matibabu zaidi baadhi wanahitaji matibabu ya haraka kwa njia ya tundu dogo ikiwemo kuwekewa betri ya moyo, wengine wanahitaji kufanyiwa matibabu ya kufungua mishipa ya damu ya moyo na wengine upasuaji wa moyo”. alisema Dkt. Eva.
Dkt. Eva alieleza kuwa idadi kubwa ya watoto waliofanyiwa uchunguzi walikuwa ni wagonjwa wapya waliogundulika kwa mara ya kwanza wakiwemo wenye matundu kwenye moyo na magonjwa ya moyo yanayojitokeza baada ya kuzaliwa.
“Baadhi ya watoto tayari walikuwa na matatizo na wakaona fursa hii waje kupimwa tena na madaktari na kuendelea na mpango wa matibabu lakini pia tulikuwa na kesi nyingi mpya ikiwemo matundu ya moyo na magonjwa ya moyo yanayopatikana baada ya kuzaliwa”, alieleza Dkt. Eva.
Kwa upande wa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watu wazima na Mshauri wa upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kutoka National Heart Institute (NHI) ya nchini Misri Prof. Ghada Kazamel alisema wingi wa wagonjwa unaonesha hitaji la kuimarisha zaidi huduma za afya ya moyo mkaoni Arusha.
“Nilishangazwa nilipofika Arusha kuona idadi kubwa ya wagonjwa, katika kambi hii tumewahudumia takribani wagonjwa 302, wengi wao wanahitaji kuwekewa betri za moyo na kufanyiwa matibabu ya uingiliaji wa mishipa ya moyo”. alisema Prof. Ghada.
Alibainisha kuwa kuna umuhimu wa Hospitali hiyo ya Ausha Lutheran Medical Centre kuwa na mtambo wa Cathlab ili kuwahudumia wananchi wa mkoa huo.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto kutoka Cairo University Children Hospital, Prof. Amal El-Sisi alisema wamewahudumia watoto kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18 wenye matatizo mbalimbali ya moyo ikiwemo ya kuzaliwa nayo.
“Tumewaona watoto wengi kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja hadi miaka 18 baadhi yao wana matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, na baadhi watahitaji kufanyiwa matibabu kwa njia ya catheter au upasuaji na matibabu hayo yanaokoa maisha”. alisema Prof. Amal El-Sisi.
Kwa upande wao wananchi wa mkoa wa Arusha waliofika kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi hiyo maalumu ya siku mbili wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo na kubainisha kuwa imewasaidia kupata uchunguzi wa mapema.
“Kwa kweli kambi hii imenisaidia sana kwa sababu imenipunguzia gharama za nauli kwenda Dar es Salaam na kurudi pamoja na gharama za malazi na maisha ya kule”. alisema Amon Emmanuel Lesilwa mkazi wa Arusha.
“Baada ya kipimo wamegundua tatizo lingine ambalo sikuwa nalijua sasa nitachukua uamuzi wa matibabu zaidi kwa kweli amenisaidia sana”, alisma Christina Kagemuro Rugakingira Mkazi wa Arusha.
Kambi hiyo ni sehemu ya mkakati wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo nchini hasa karibu na wananchi.