Afya kwanza: JKCI yahakikishia usalama wa mioyo ya wanamichezo Chipukizi Cup Arusha
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Friday, Dec 19, 2025
Zaidi ya wanamichezo 176 wamenufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika mashindano ya 16 ya Chipukizi Cup yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) jijini Arusha.
Zoezi hilo la siku nne limekuwa msaada mkubwa kwa wanamichezo chipukizi, kwa kuwa limewasaidia kutambua mapema hali za afya ya mioyo yao na kuepuka hatari ya kupata matatizo ya moyo yanayoweza kujitokeza ghafla wakati wa mazoezi makali au mashindano.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka JKCI, Hospitali ya Dar Group Dkt. Eva Wakuganda alisema wanamichezo waliopatiwa huduma hizo wanatoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda na Zimbabwe.
Alisema uchunguzi wa awali wa afya ya moyo ni hatua muhimu kwa wanamichezo hasa katika mashindano makubwa, kwani baadhi yao huzaliwa na matatizo ya moyo yasiyoonekana kwa macho lakini yanaweza kusababisha madhara makubwa wanapofanya mazoezi makali.
“Mazoezi yana faida nyingi kiafya; huimarisha afya ya mwili, huongeza uwezo wa kufikiri na hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Hata hivyo faida hizo hupatikana zaidi endapo uchunguzi wa afya utafanyika mapema,” alisema Dkt. Eva.
Hata hivyo alisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa kiafya kabla ya kushiriki michezo ya ushindani.
“Tunashauri wanamichezo wafanyiwe uchunguzi na wenye matatizo wapatiwe matibabu ya moyo kabla ya kushiriki mazoezi makali au mashindano, ili kubaini mapema viashiria vyovyote vinavyoweza kusababisha madhara au vifo vya ghafla viwanjani,” aliongeza.
Kwa upande wake mchezaji kutoka Future Star Academy ya jijini Arusha Arusha, Paschal Bugeraha alisema huduma hiyo imewajengea uelewa wa magonjwa ya moyo na kujiamini zaidi.
“Upimaji huu umetusaidia kujua hali za afya ya mioyo yetu na kupata elimu kuhusu dalili za magonjwa ya moyo. Endapo tutaziona dalili hizo, tutaweza kuchukua hatua mapema,” aalisema Bugeraha.
Naye mchezaji kutoka Kilimanjaro Alice Emmanuel aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma bora na za kitaalamu za magonjwa ya moyo.
“Huduma za moyo zinazotolewa na JKCI ni za kiwango cha juu. Madaktari akiwemo Dkt. Eva na timu yake, wametupokea vizuri na kutuhudumia kwa weledi mkubwa,” alisema.
Zoezi la uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wanamichezo katika mashindano ya 16 ya Chipkiz Cup linafanyika kuanzia tarehe 15 hadi 21 Desemba 2025 katika viwanja vya michezo vya Tanganyika Game Trackers (TGT) mkoani Arusha.