Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Wagonjwa watano wenye mishipa ya damu iliyoziba kwa asilimia 75 kufanyiwa upasuaji wa moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Dec 17, 2025
image description

Wagonjwa watano wenye mishipa ya damu iliyoziba kwa asilimia zaidi ya 75 kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo bila kusimamisha moyo (off – Pump CABG).

Upasuaji huo unafanyika katika kambi maalumu ya siku tano iliyoanza jana na kufanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo ni maalumu kwa wagonjwa ambao mishipa yao ya moyo imeziba hivyo kusababisha ufanyaji kazi wa mioyo yao kuwa chini ya asilimia 35.

“Wagonjwa tunaowafanyia upasuaji katika kambi hii mara nyingi utuchukua ugumu kidogo kuwafanyia upasuaji kutokana na ufanyaji kazi wa mioyo yao, hivyo ili waweze kuwa na matokeo mazuri mara nyingi wenzetu wanafanya upasuaji huu bila ya kuusimamisha moyo kama ambavyo tunaenda kufanya katika kambi hii”, alisema Dkt. Angela

Dkt. Angela alisema kupitia kambi hiyo wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watajengewa uwezo ambao utasaidia kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kwa wagonjwa ambao mioyo yao imechoka kutokana na kuziba kwa mishipa ya damu kwa asilimia zaidi ya 75.

“Kambi hii itakuwa endelevu mpaka pale wataalamu wetu watakapoweza kutoa huduma hii bila ya kuusimamisha moyo kwani wagonjwa wanaohitaji huduma hii ni wengi lakini kutokana na hali zao tumekuwa tukiwaweka kwenye matibabu ya dawa kwa muda mrefu kusaidia kuboresha ufanyaji kazi wa mioyo yao”, alisema Dkt. Angela

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India Upendra Bhalerao alisema ameona aungane na wataalamu wa JKCI kuwasaidia wagonjwa ambao kutokana na matatizo ya mishipa ya damu kuziba kwa asilimia zaidi ya 75 wanashindwa kujishughulisha na wakati mwingine hupoteza maisha.

“Wagonjwa tutakaowafanyia upasuaji kupitia kambi hii wataweza kufanya shughuli ndogondogo ambazo hapo awali walikuwa hawezi kuzifanya”, alisema Dkt. Bhalerao 

Dkt. Bhalerao alisema kupitia kambi hiyo wataalamu watatoa huduma sambamba na kupata mafunzo yatakayosaidia kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na matatizo ya mishipa ya damu ya moyo kuziba.

“Tutaendelea kushirikiana na Taasisi hii na kuweka kambi za matibabu ya mishipa ya damu mara kwa mara ili ujuzi huu uweze kuwafikia wataalamu wa JKCI na hapo baadaye waweze kufanya upasuaji wa namna hii bila ya kuusimamisha moyo”, alisema Dkt. Bhalerao

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Health & Wellness Companion Ltd (HWC) iliyofanikisha ujio wa wataalamu hao Dkt. Priyank Punatar alisema ujio wa wataalamu hao unaakisi dhamira ya pamoja ya kuwezesha huduma bingwa za kiwango cha kimataifa kuwafikia wataalamu wote. 

Dkt. Punatar alisema kupitia ushirikiano huo wamelenga kufikisha huduma za juu za upasuaji wa moyo kupatikana kwa urahisi, kwa gharama nafuu, na kwa karibu bila kulazimika kusafiri nje ya nchi.

“HWC tunaamini huduma bora za afya ni haki ya kila mtu na si fursa kwa wachache, kambi hii ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa huduma za afya nchini huku tukihakikisha wagonjwa wetu wanapata huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa”, alisema Dkt. Punatar