“Alikuwa Taa Yetu”: JKCI Yamkumbuka Patrick kwa maono yake makubwa
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Dec 17, 2025
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, unyenyekevu, utulivu na moyo wa kujitolea ili kuendeleza maendeleo ya taasisi hiyo na kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge wakati wa misa ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Afisa TEHAMA wa taasisi hiyo marehemu Patrick Agustino Ngalawa kijana aliyewagusa wengi kwa moyo wake wa kujitolea na tabia za kipekee.
Dkt. Kisenge alisema Patrick kijana wenye umri wa miaka 30 alikuwa mstari wa mbele katika kazi, alifanya yote kwa moyo wa dhati na hakupenda makuu wala kujitafutia sifa. Alitumia maisha yake yote kusaidia JKCI na wananchi wanaotegemea huduma za taasisi hiyo.
“Leo tunayaenzi maisha ya kijana wetu Patrick. Ametuacha mapema lakini mchango wake kwa taasisi ni mkubwa. Ameonesha uadilifu, unyenyekevu na moyo wa kujitolea wakati wote alipohitajika,” alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa Patrick alikuwa taa ndogo iliyoangaza katika mazingira magumu ya kazi. Alianzisha mifumo mbalimbali ya TEHAMA iliyoleta tija katika utoaji wa huduma, ikiwemo mfumo wa kidigitali wa kufanya miadi ya kuonana na daktari.
“Kazi ya mikono yake itaendelea kuishi ndani ya taasisi yetu. Tabia yake iwe mfano kwetu. Katika kulienzi jina lake, tutaanzisha mfuko wa ubunifu utakaojulikana kwa jina la Patrick Agustino Ngalawa utakaotoa motisha kwa wafanyakazi watakaofanya ubunifu”.
“Pia kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo (CardioTan) wa 2026 na 2027, asilimia 1 ya makusanyo ya mkutano huo ipelekwe kwa familia yake kusaidia malezi ya mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MNH alikuwa Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI alisema Patrick alikuwa kijana wa maono makubwa mchapakazi na mzalendo aliyeacha alama isiyofutika.
“Hakika moto wa maarifa aliouwasha utaendelea kuwaka kwa muda mrefu. Aliamini kwenye ubunifu wa teknolojia kama chombo cha kuokoa maisha ya watu na alikuwa mwanaharakati wa afya na msimamia maono, mchango wake wa kuhamasisha mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo ni urithi wake kwa taifa,” alisema Dkt. Delilah.
“Katika mkutano wa CardioTan 2025 ambao mimi nilikuwa Mwenyekiti, Patrick ameweka alama kwa kuandaa tovuti ya mkutano mkubwa wa kimataifa wa magonjwa ya moyo na kutoa mchango mkubwa wa uhamasishaji wa mkutano huo uliolenga kuzuia na kutibu magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Delilah.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MOI alikuwa Daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi wa JKCI, alisema marehemu Patrick alikuwa mfano wa aina ya watumishi wanaoifanya sekta ya afya isonge mbele, watu wenye maono, weledi na moyo wa kuitumikia nchi bila kutafuta makuu.
Alisema Patrick aliweka alama isiyofutika katika kazi yake na mchango wake unaendelea kuonekana hata baada ya kuondoka.
Balozi Dkt. Mpoki aliongeza kuwa njia bora ya kumuenzi Patrick ni kuendeleza yale aliyoyaamini: ubunifu, kufanya kazi kwa uadilifu na kuikumbatia teknolojia kama nyenzo ya kuboresha huduma za afya.
Wakimzungumzia marehemu Patrick wafanyakazi wa JKCI walisema kijana huyo hauhitaji nguvu nyingi kumsifia na kumpamba kwani amekuwa wa kipeke ambaye ameonesha weledi mkubwa, kuwa mfano mzuri wa imani na kuwa tayari kusaidia wakati wowote hata kama ni kazi binafsi.
“Alikuwa mwaminifu, ana nidhamu na mwepesi kusaidia, alichangia sana maendeleo ya kazi za kitengo na Taasisi, matendo na maisha ya Patrick yamekuwa kioo ambacho kila mtu angependa kuwa”, alisema Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI Dkt. Tatizo Waane.
“Tunamshukuru Mungu kwaajili ya familia yake kwa kumlea na kumfikisha hapa, ameishi maisha kamili, alionesha upendo katika kazi, uwezo wa kuleta majawabu na kuhakikisha wenzake wanaelewa wakati wote wa kuandaa mifumo ya Taasisi, kutokana na weledi wake ilinifanya nimpende sana”, alisema Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa JKCI Lazaro Swai.
Marehemu Patrick ameacha alama kubwa JKCI kupitia ubunifu wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA, ambayo imesaidia sana kuboresha huduma za moyo kwa wagonjwa. Kifo chake kimeacha pengo, lakini maadili yake ya uadilifu, ubunifu na kujitolea vitabaki kuwa fundisho kwa kila mfanyakazi wa JKCI na taifa kwa ujumla.