Huduma za JKCI Dar Group Kuboreka Kupitia Ujenzi wa Jengo la Kisasa
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Tuesday, Nov 25, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepanga kuboresha huduma zake kwa kujenga jengo jipya la kisasa katika tawi lake la Hospitali ya Dar Group, hatua inayolenga kupanua na kuongeza ubora wa matibabu kwa wananchi.
Jengo hilo jipya linalotarajiwa kuanza kujengwa mwakani litaboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya wagonjwa wa moyo, sambamba na kuwa kituo maalum cha kuwahudumia wanamichezo kutoka vilabu vinavyoshiriki michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) pamoja na vile vya Ligi Kuu na mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Akizungumza kwenye kikao cha ndani na wafanyakazi wa Hospitali ya JKCI Dar Group, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge alisema uboreshaji huo wa miundombinu utaiwezesha hospitali kutoa huduma bora na za uhakika zaidi.
Aliwataka wafanyakazi kuwa wabunifu na kuwasilisha mapendekezo ya maboresho mbalimbali ili kwa pamoja kuhakikisha tawi hilo linakuwa kituo cha mfano katika utoaji wa huduma za tiba.
“Mnapaswa kufanya kazi kwa bidii, kutoa huduma bora, kuwa wavumilivu na kutekeleza majukumu yenu kwa weledi ili tufikie mafanikio tunayokusudia. Ujenzi na mafanikio ya tawi hili ni jukumu letu sote", alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema tayari tawi hilo limeanza hatua za awali za maboresho kwa kukarabati baadhi ya maeneo ili kuipa hospitali mandhari ya kisasa.
“Tumeanza kwa kukarabati chumba cha upasuaji, kuanzisha wodi za watu maalumu (VIP Wards), kukarabati chumba cha mikutano na kwa sasa tunaendelea na ukarabati wa ofisi za watumishi pamoja na eneo la wagonjwa wa nje (OPD) ", alisema Dkt. Shemu.
Aliongeza kuwa wafanyakazi wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa malengo kwa kuwa matokeo ya juhudi zao yanaonekana kupitia mafanikio yanayoipatia heshima taasisi.
Baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo walipongeza mpango huo, wakisema utaongeza tija na kurahisisha kazi zao za kila siku.
Muuguzi wa wodi ya wagonjwa wa nje Fatna Syedt alisema kwa sasa wanahudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja. Jengo jipya litasaidia kupunguza msongamano na kuongeza faraja kwa wagonjwa kwani watawafikia watu wengi zaidi bila kuchelewesha huduma.
Mtaalamu wa uchunguzi wa moyo (echo), Eliza Shuma naye alisema vifaa vya kisasa vitawaongezea ufanisi. Kuna wakati wanalazimika kusubiri chumba kiwe wazi ili kuendelea na vipimo wakipata nafasi mpya tutahudumia watu kwa haraka na utapunguza presha ya kazi na kutoa huduma bora zaidi.