Hatua kubwa JKCI – yazindua kitengo cha kisasa cha Dialysis kwa wagonjwa wa moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Nov 12, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imezindua rasmi kitengo kipya cha kusafisha damu (dialysis unit) kwa wagonjwa wa moyo wanaopata matatizo ya figo hatua inayolenga kuboresha huduma za tiba jumuishi kwa wagonjwa hao.
Kitengo hicho chenye mashine za kisasa zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 kilichozinduliwa jana kimeanza kutoa huduma mara moja baada ya kuzinduliwa huku kikiwa na uwezo wa kusafisha damu kwa zaidi ya wagonjwa nane kwa siku.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema uanzishwaji wa kitengo hicho umetokana na ongezeko la wagonjwa wa moyo wanaokabiliwa na matatizo ya figo hali iliyokuwa ikiwalazimu kwenda kupata huduma hiyo katika hospitali nyingine.
“Wagonjwa wengi wa moyo hupata matatizo ya figo kutokana na hali zao za kiafya au matibabu wanayopata. Awali walikuwa wanachelewa kupata huduma kwa sababu ya wingi wa wagonjwa katika hospitali nyingine, lakini sasa huduma hiyo itapatikana hapa hapa JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo aliongeza kuwa kuanzishwa kwa kitengo hicho ni sehemu ya mpango wa JKCI wa kuhakikisha huduma zote muhimu kwa wagonjwa wa moyo zinapatikana chini ya paa moja, hatua itakayoongeza ufanisi na kurahisisha matibabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema awamu ya kwanza ya kitengo hicho ina vitanda viwili huku mpango wa muda mrefu ukiwa ni kuongeza hadi zaidi ya vitanda 20 ili kuhudumia wagonjwa wengi zaidi.
“Tunafurahia kuona huduma hii inaanza rasmi JKCI. Wagonjwa wetu sasa watapata huduma za moyo na figo mahali pamoja jambo litakalopunguza usumbufu na kuboresha matokeo ya matibabu”, alisema Dkt. Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi.
Naye Daktari bingwa wa figo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Daniel Msilanga ambaye anatoa huduma za matibabu ya figo kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo alisema kufunguliwa kwa kitengo hicho kutarahisisha upatikanaji wa huduma za figo kwa wagonjwa wa moyo ambao awali walikuwa wakihangaika kupata huduma hiyo nje ya taasisi.
“Tumeona ongezeko kubwa la wagonjwa wenye matatizo ya moyo na figo. Kitengo hiki kitasaidia kupunguza msongamano katika hospitali nyingine na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma”, alisema Dkt. Msilanga.
Kwa upande wake msimamizi wa kitengo hicho cha figo Daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nai Kipuyo alisema kitengo hicho kinaendeshwa na timu ya wataalamu waliobobea wakiwemo madaktari, wauguzi na mafundi sanifu waliopata mafunzo maalum ndani na nje ya nchi kwa ushirikiano na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Uzinduzi wa kitengo hicho umeenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo JKCI imetoa wito kwa wananchi kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya zao, hasa magonjwa ya moyo na figo ambayo yanaendelea kuongezeka kwa kasi duniani.