Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Wahasibu JKCI wagusa mioyo ya wagonjwa

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Nov 12, 2025
image description

Jamii imetakiwa kujenga utamaduni wa kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali wakiwemo wagonjwa, wazee na makundi mengine yenye uhitaji maalumu ili kukuza mshikamano na utu.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Agnes Kuhenga wakati akikabidhi zawadi kwa watoto wenye matatizo ya moyo wanaotibiwa katika taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahasibu.

CPA. Agnes alisema wahasibu wa JKCI waliamua kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya jambo la kijamii ili kuwafariji wagonjwa na kuonesha moyo wa upendo kwa jamii.

“Tumetoa zawadi mbalimbali zikiwemo nepi, sabuni, mafuta, sukari, biskuti na juisi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni mbili.

“Tuliona katika kuadhimisha siku hii tujichangishe fedha na kununua mahitaji ya watoto, ni vyema tukawagusa wagonjwa wanaopokea huduma katika taasisi yetu, hasa watoto wenye matatizo ya moyo”, alisema CPA. Kuhenga.

Aliongeza kuwa wagonjwa wengi wanaotibiwa JKCI wanatoka mikoani na baadhi yao kutoka familia zenye kipato cha chini, hivyo msaada huo ni njia ya kuwafariji na kuwapa matumaini mapya wakati wa matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliwapongeza wahasibu wa taasisi hiyo kwa moyo wa upendo na kujitolea, akisema kuwa kitendo hicho ni cha kuigwa na idara nyingine ndani ya taasisi.

“Ni jambo la kufurahisha kuona wahasibu wetu wakitumia siku yao ya kimataifa kuwasaidia wagonjwa wanaowahudumia kila siku. Kwa kawaida tumekuwa tukipokea msaada kutoka makundi ya nje, lakini leo tumepokea msaada kutoka ndani ya familia ya JKCI. Huu ni mfano mzuri wa uzalendo na utu wa kweli”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo, alisema wahasibu ni nguzo muhimu katika mafanikio ya taasisi yoyote kwa kuwa usimamizi mzuri wa fedha unaiwezesha taasisi kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Tangu kuanzishwa kwa taasisi hii mwaka 2015, JKCI imekuwa ikipata hati safi za ukaguzi kila mwaka kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Hii ni ishara ya uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu walionao wahasibu wetu”, alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa usimamizi mzuri wa fedha umeiwezesha JKCI kupanua huduma zake na kuifikia zaidi ya mikoa 22, kupitia kliniki za moyo zinazowafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao.

Naye Mkuu wa Kitengo cha  Uhasibu wa JKCI CPA. Reuben Nyiti alisema maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Kukuza Uwajibikaji na Utendaji Bora Kupitia Teknolojia na Uchangiaji kwa Jamii” ambayo inalenga kuwahamasisha watumishi kufanya kazi kwa bidii huku wakikumbuka kuwajali wanaowahudumia.

“Tunatambua wagonjwa wetu wanatoka sehemu mbalimbali za nchi, hivyo ni wajibu wetu kuonesha upendo, huruma na mshikamano.Tumeamua kutumia siku yetu kama wahasibu kuwa karibu na wagonjwa badala ya kusherehekea tukiwa ofisini”, alisema CPA. Nyiti.

Nao wazazi wa watoto waliopokea zawadi hizo hawakuficha furaha yao, wakieleza kuwa msaada huo umeleta faraja kubwa kwao na kuwapa matumaini mapya wakati watoto wao wakiendelea na matibabu.

“Tumejawa na furaha kubwa, leo hii tumeguswa kwa upendo.Tunawashukuru wahasibu wa JKCI kwa moyo wao wa utu na kujali”, alisema Sophia Albano mkazi wa Mtwara ambaye mtoto wake anatibiwa katika taasisi hiyo.

Sophia alisema zawadi walizopewa si tu msaada wa mahitaji ya kila siku, bali pia ni ishara ya upendo unaoonesha kuwa jamii bado inajali wagonjwa na familia zao.

“Zawadi hizi zimeleta tabasamu, hasa kwa watoto wanaopitia matibabu magumu. Ni jambo dogo kwa wengine, lakini kwetu lina maana kubwa sana”.

“Tumefarijika sana kwa zawadi hizi. Hii ni ishara ya kuwa familia yetu haiko peke yake katika changamoto hizi. Tunapenda kuwashukuru wahasibu wote wa JKCI kwa moyo wao wa huruma na kujali”, alisema Lilian Mwita mkazi wa Dar es Salaam  ambaye mtoto wake anatibiwa katika taasisi hiyo.