Moyo Wangu, Afya Yangu: JKCI na HTAF wazindua shindano la insha kwa wanafunzi
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Oct 02, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) wameanzisha shindano la insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini kuwaelimisha kuhusu magonjwa ya moyo.
Shindano hilo yenye kauli mbiu isemayo “Moyo wangu afya yangu” ni sehemu ya mradi wa miaka mitatu wa Taasisi hiyo unaolenga kuongeza uelewa na kukuza kinga ya magonjwa yasiyoambukiza hususani magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa watoto wenye umri wa kwenda shule.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shindano la uandishi wa insha Shule za Sekondari kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo Kamishina wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa alisema mradi huo unatarajia kutoa elimu na kuwafikia watoto wa shule za sekondari kwa kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu unakuwa endelevu na kuwafikia wanafunzi wengi nchini
“Kupitia mradi huo kutakuwa na vilabu vya afya mashuleni, vipeperushi vinavyotoa elimu ya magonjwa ya moyo, vijarida, mabango, mashindano ya uandishi wa insha, midahalo, kampeni za afya na usafi wa mazingira”, alisema Dkt. Mtahabwa
Dkt. Mtahabwa alisema mbinu zote hizo zitatumika kama majukwaa ya kuwaelimisha na kuwashirikisha wanafunzi kwa kuwajengea uwezo waweze kufahamu umuhimu wa afya na namna ya kujikinga na magongwa ya moyo.
“Rasilimali watoto ni rasilimali yenye thamani kubwa kuliko rasilimali nyingine yeyote na haina mbadala wake, juhudu za watanzania zielekezwe katika kumlinda mtoto kuhakikisha yuko salama na katika mazingira rafiki ili aweze kufikia ustawi tarajali”, alisema Dkt. Mutahabwa
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema jamii sasa imekuwa na mtindo wa maisha ambao si mzuri kwa watoto kwa kuwapa vyakula ambavyo havizingatii mtindo bora na ulaji wenye lishe bora hivyo JKCI na HTAF zikaona ili kuzuia magonjwa ya moyo kwa watoto waanzishe mradi huo kuwapa elimu ya kutosha watoto waweze kupenda afya zao.
“Kama mtoto wako hali lishe bora atakavyokuwa mkubwa atakuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo, JKCI tunasherehekea mafanikio ya miaka 10 sio kwa kutoa huduma kwa wagonjwa wengi bali tunataka pia kuongeza jitihada katika kuilinda jamii isipate magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema shindao la isha linabeba dhamana ya kukuza uwezo wa wanafunzi katika kuelewa na kueleza masuala ya afya ya moyo kwa maandishi ili waweze kuielimisha jamii, kugundua na kukuza vipaji vya uandishi miongoni mwao na kuwafanya wanafunzi kuwa mabalozi wa afya katika taifa.
Naye Mtendaji Mkuu wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani alisema JKCI na HTAF wanataka kupeleka elimu ya moyo mashuleni wakiwa na nia ya kusaidia watoto ili pale wanapokuwa wasikumbane na changamoto ya magonjwa ya moyo.
“Tumegundua kuwa magonjwa mengi ya moyo ambayo watu wazima wanapata chanzo chake uanzia utotoni, hivyo tukaona ni muhimu kupeleka elimu hii ya afya ya moyo mashuleni kuwawezesha watoto wapate elimu ya afya ya moyo”, alisema Dkt. Naiz
Washindi wa shindalo hilo linaloanza rasmi tarehe 8 Oktoba hadi 1 Novemba 2025 watapewa zawadi ambapo mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 3 na laptop, mshindi wa pili atapata shilingi milioni 2 na laptop, mshindi wa tatu atapata shilingi milioni 1 na tablet, mshindi wa nne atapata shilingi laki 5 na cheti na mshindi wa tano atapata shilingi laki 3 na cheti.
Sambamba na zawadi hizo washindi hao pia watapewa nafasi ya kujengewa uwezo wa kushirikiana katika miradi ya elimu ya afya ya moyo ili kupitia kwao ujumbe kuhusu kinga ya afya ya moyo uweze kwenda kwa kasi na kuifikia jamii yote.