Kampuni ya Huduma za Kifedha ya ASA Microfinance kwa kushirikiana na Benki ya CRDB zatoa baiskeli 30 za wagonjwa JKCI.
Author:JKCI Admin
Published At:Wednesday, Sep 03, 2025
Kampuni ya Huduma za Kifedha ya ASA Microfinance kwakushirikiana na Benki ya CRDB zatoa baiskeli 30 za wagonjwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kusaidia wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa kupokea viti hivyo leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi wa JKCI Robert Mallya alisema baiskeli hizo zitasaidia katika kurahisisha mzunguko wa wagonjwa wanaoingia na kutoka JKCI.
“Tunawashukuru sana Kampuni ya Huduma za Kifedha ya ASA Microfinance na Benki ya CRDB kwa kuona umuhimu wa kuwajali wagonjwa wetu hivyo kuamua kutuletea baiskeli hizo 30”, alisema Mallya
Mallya alisema JKCI ina wagonjwa wengi ambao wanahitaji kuzungushwa na baiskeli ili kufika katika maeneo ya kupata huduma hivyo viti mwendo hivyo vitasaidia kurahisisha huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji kutoka Kampuni ya Huduma za Kifedha ya ASA Microfinance Muhammad Shah Newaj alisema mbali na kutoa huduma za fedha pia wamejikita katika kusaidia jamii kwa kutoa vifaa tiba ili kupunguza baadhi ya changamoto zinazo ikabili sekta ya afya.
“Huu ni mwanzo katika kusaidia wagonjwa wa moyo ambao wanahitaji mizunguko ya kwenda katika maeneo tofauti kupata huduma na vipimo, tutaendelea kuwafikia na kuwapa mahitaji tofauti”, alisema Muhammad
Mohammad alisema kampuni ya Huduma za Kifedha ya ASA iliona mwaka huu irejeshe kwa jamii faida inayopata kwa kutoa baiskeli hizo kwa wagonjwa wa moyo wanaotibiwa JKCI.
Naye Meneja Mwandamizi uwekezaji kwa jamii CRDB Benki Foundation Ninael Munuo alisema lengo la ushirikiano huo na kampuni ya ASA ni kuleta matumaini kwa wagonjwa kwa kuwapatia mahitaji muhimu wanayohitaji wanapokuwa hospitali.
“Kupitia mbio za nyika zinazofanwa na Benki ya CRDB tumekuwa tukiwapa kipaumbele watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibwa JKCI hivyo tukaona sasa tushirikiane na ASA katika kuleta matumaini kwa wagonjwa wa JKCI wanaohitaji baiskeli kwenda sehemu tofauti wakati wa matibabu”
Tasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikishirikiana na Taasisi mbalimbali zikiwemo za fedha katika kuboresha huduma bingwa bobezi za magonjwa ya moyo nchini.