• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Tanzania yashiriki maonesho ya 79 ya Kilimo na Biashara ya Zambia

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Jul 30, 2025
image description

Tanzania inashiriki katika maonesho ya 79 ya Kilimo na Biashara ya Zambia ikiwa na lengo la kutangaza huduma za matibabu ya ubingwa bobezi zinazopatikana nchini pamoja na huduma za usafirishaji.

Hayo yamesemwa leo na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusu nchi hiyo kushiriki katika maonesho hayo yanayofanyika jijini Lusaka.

Alisema kwa mara ya kwanza Taasisi kubwa tano zinazotoa huduma za afya na usafirishaji zimeshiriki katika maonesho hayo na hivyo Tanzania kupata nafasi ya kutangaza huduma inazozitoa kwa wananchi wa Zambia na washiriki wa maonesho hayo.

“Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia umeratibu ushiriki wa taasisi zetu kubwa tano katika maonesho haya ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MRRH), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Ndege la Air Tanzania”.

“Serikali yetu imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ikiwemo kujenga majengo ya kisasa, kununua vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalamu katika ngazi ya ubingwa bobezi, kushiriki kwa taasisi hizi katika maonesho haya kutawawezesha kutangaza huduma wanazozitoa na wagonjwa wengi kuja kutibiwa katika nchi yetu na  kutuingizia fedha za kigeni’, alisema Mhe. Balozi Luteni Generali Mkingule.

Alisema wafanyabiasha wengi wa Zambia wanakuja nchini kununua bidhaa na wengine wanakwenda nje ya nchi imefika wakati sasa kwa wafanyabiashara hao kutumia bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kuu la biashara katika nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kusafirisha mizigo yao  na wasafiri kwa kutumia Shirika la ndege la  Air Tanzania ambalo ndege zake zinakwenda katika nchi za SADC.

Kwa upande wa washiriki wa maonesho hayo walishukuru kwa kupata nafasi ya kushiriki katika maonesho hayo na kusema kuwa wamejipanga kutangaza huduma zinazotolewa katika taasisi zao ili wananchi wa Zambia na mataifa mengine yanayoshiriki katika maonesho hayo waende Tanzania kufuata huduma hizo pia watumie huduma hizo pale watakaposafiri au kusafirisha mizigo yao.

“Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inashiriki katika maonesho ya 79 ya Kilimo na Biashara ya Zambia kwa kutangaza huduma za matibabu ya moyo tunazozitoa, kutoa elimu ya magonjwa ya moyo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa watu wenye matatizo ya moyo”.

“Taasisi yetu ni moja ya taasisi bora barani Afrika inayotoa huduma za ubingwa bobezi wa matibabu ya moyo, tumejipanga kuwafikia wagonjwa wengi zaidi ndani na nje ya nchi na ndiyo maana tuko hapa kutangaza huduma ya utalii wa matibabu ambayo inapatikana nchini kwetu”, alisema Dkt. Alex Joseph ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu.

“Tunafurahi kushiriki katika maonesho haya ya 97 ya Kilimo na Biashara hapa Zambia, tunatumia nafasi hii kutoa ushauri wa kibingwa bobezi kwa wananchi wa Zambia na washiriki wote wa maonyesho haya na kutangaza kliniki yetu ya wagonjwa maalumu (VIP) na wa Kimataifa inayopatikana katika Taasisi yetu  ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI)”, alisema Daktari bingwa wa mifupa Joseph Lamtane.

 “Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MRRH) inashiriki katika maonesho haya kwa kutangaza huduma za matibabu ya ubingwa bobezi tunazozitoa katika hospitali yetu huduma hizo ni pamoja na matibabu ya saratani, kwa kuwa Mbeya ni karibu na Zambia ninaamini baanda ya maonesho haya wagonjwa wengi kutoka Zambia watakuja kutibiwa”, alisema Daktari bingwa wa upasuaji kwa watoto Lazaro Mboma.