JKCI yaihamasisha jamii kupata chanjo ya homa ya ini
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Friday, Jul 11, 2025
Jamii imehamasishwa kujitokeza kufanya kipimo na kupata chanjo ya ugonjwa wa homa ya ini ambao umekuwa tatizo kubwa katika jamii kwani virusi vya homa hiyo vipo na vinaambukiza kwa kasi.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa usalama mahala pa kazi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elias Birago wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA).
Dkt. Birago alisema virusi vya homa hiyo vinaambukiza kwa njia ya majimaji yanayotoka katika mwili wa binadamu mwenye maambukizi ikiwemo damu, jasho, maji ya uzazi “Amniotic fluid”, kujamiiana pamoja na matumizi ya vifaa vyenye ncha kali vilivyotumika kwa mgonjwa wa homa ya ini.
“Lengo letu kubwa kutoa huduma hii katika maonesho ya Sabasaba ni kuikinga jamii isipate maambukizi ya homa ya ini, wale tutakaowapima na kuwakuta na shida tutawaelekeza namna nzuri ya kupata matibabu na kwa wale ambao wako salama watapata chanjo kupitia maonesho haya”, alisema Dkt. Birago
Dkt. Birago alisema dalili za awali za ugonjwa huo zinaweza zisionekane lakini ugonjwa unavyoendelea mtu anaweza kupata manjano, mwili kuchoka, ngozi kuwasha, kupata homa, kupungua uzito hivyo kupeleka ini kushindwa kufanya kazi.
“Tumeweza kutoa elimu na umuhimu wa kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini kwa jamii kupitia maonesho haya kuiwezesha jamii kujua tatizo hilo kuwa lipo na halina dawa lakini lina kinga iwapo mtu atafanya kipimo na kupata chanjo yake”, alisema Dkt. Birago
Dkt. Birago alisema JKCI kupitia kitengo cha Usalama mahala pa kazi kilichopo Hospitali ya Dar Group wamekuwa wakitembelea taasisi na mashirika mbalimbali kwaajili ya kutoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini.
Kwa upande wake Afisa Uuguzi wa Taasisi hiyo Florah Kasema alisema wananchi waliotembelea banda la JKCI wamehamasika kupata chanjo hiyo ambayo wengi wao hawakuwa wakifahamu madhara yake.
Florah alisema ugonjwa wa homa ya ini unaongezeka kwa kasi na kuathiri jamii hivyo wataalamu wa JKCI hawataishia kutoa huduma hiyo katika maonesho ya Sabasaba bali wataendelea kutoa elimu na chanjo hiyo katika vituo vyao vya afya.
“Ni muhimu wale wote walioanza kupata chanjo ya homa ya ini kuhakikisha wanamaliza chanjo hiyo kwa kupata chanjo zote tatu kwa kipindi cha miezi sita kama ambavyo wameshauriwa na wataalamu wa afya”, alisema Florah