• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Makonda aishukuru JKCI kwa kufanya upimaji wa moyo kwa wakazi wa Arusha

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jul 03, 2025
image description

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amewashukuru wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi wa mkoa huo  kupitia kambi maalumu ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Pongezi hizo amezitoa jana  alipotembelea kambi hiyo ya matibabu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha

Makonda alisema mchango wa taasisi hiyo wa kuboresha afya za wananchi wa Arusha ni wa kipekee kwa kuwa imewasaidia watu wengi  kupata huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo ambazo ilibidi  wasafiri na kuzifuata jijini  Dar es Salaam.

“Ninawashukuru madaktari kwa moyo wa kujitoa waliouonyesha kwa wananchi wa Arusha na ninawapongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya”, alisema Makonda.

Makonda alitumia fursa hiyo pia kuwaaga madaktari wa JKCI na kuwaomba waendelee kuwahudumia wananchi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi bila ya kuangalia tofauti ya vipato vyao.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aloyce Mohamed alimshukuru Makonda kwa moyo wake wa kujitoa wa kuhakikisha wananchi wa Arusha wanapata huduma bora za matibabu ya moyo.

Kambi hiyo ya siku saba inalenga kutoa huduma za upimaji na ushauri wa kitaalamu wa magonjwa ya moyo kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Arusha na mikoa jirani ikiwa ni sehemu ya kampeni ya serikali ya kuhamasisha utunzaji wa afya.