• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

iongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuulinda utamaduni wa taasisi hiyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jul 03, 2025
image description

Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuulinda utamaduni wa taasisi hiyo wa kuwahudumia wagonjwa kwa kiwango cha juu cha uadilifu na weledi kwa kufanya hivyo watu wengi zaidi watafaidika na huduma wanazizitoa.

Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wa jinsi ya kutekeleza majukumu yao ya kazi viongozi wa taasisi hiyo yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo wilayani humo.

Mhe. Simon alisema utamaduni wa taasisi yoyote ile unaweza kusababisha taasisi ikafanya kazi vizuri au ikaanguka hii inategemea na jinsi ambavyo wanatoa huduma kwa wateja wao.

“Utamaduni wa taasisi unauona pale ambapo wafanyakazi wake wanawapokea wateja wao na kuwahudumia ni muhimu kila mfanyakazi akafahamu utamaduni mlionao na kuulinda kwani utamaduni wenu ukibadilika na kuwa mbaya inaweza kusababisha tasisi ikaanguka”, alisema Mhe. Simon.

Mhe. Simon aliwapongeza viongozi hao kwa huduma bora wanayoitoa ya kuokoa maisha ya kwa wagonjwa wa moyo wanaowatibu wa ndani na nje ya nchi.

“Kazi mnayoifanya ni kubwa ya kuokoa maisha ya watu ninawaomba muendelee na moyo huo huo msikate tamaa kwani wagonjwa wanawategemea muwatibu, wapone na kuendelea na maisha yao ya kawaida”, alisema Mhe. Simon.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge alisema mafunzo hayo kwa viongozi yatawajengea uwezo wa kufanya kazi zao kimkakati na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu kwa kufuata miongozo na taratibu zilizopo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema ili kuwapata viongozi wazuri  ni  lazima waandaliwe,  wajitoe kufanya kazi kwa bidii na wawe wazalendo kwani kila mtu akifanya kazi vizuri watafikia malengo waliyojiwekea kuwa moja ya taasisi bora za  kimataifa.

“JKCI ni moja ya taasisi kubwa Afrika Mashariki na Kati inahudumia wagonjwa kutoka nchi zaidi ya 20, tunavyowapokea wagonjwa kutoka nchi za nje wanafanya utalii tiba na hivyo kuiongezea nchi yetu mapato”.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika taasisi yetu kwani tuna vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wa kutosha ambao wanatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wagonjwa”, alisema Dkt. Kisenge.

Naye Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia alisema mada ya utaifa na uzalendo ambayo aliwafundisha viongozi hao imewafanya waelewe umuhimu wa taasisi yao kwa ustawi wa nchi na wananchi kwani wanaziba pengo lililokuwepo miaka ya nyuma la kuwapeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi.

“Nimewakumbusha kuilinda misingi ya utaifa na uzalendo ambayo inawaongoza  katika utumishi wa umma kwani vitu hivi viwili  ndivyo vilivyoifanya nchi yetu kuwa na amani na usalama”, alisema Kanali Mstaafu Simbakalia.

Nao viongozi walioshiriki katika mafunzo hayo walishukuru kwa kupata nafasi hiyo na kusema kuwa yale waliyojifunza watakwenda kuyafanyia kazi ili kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi.

“Mafunzo niliyoyapata ni mazuri yatanisaidia katika utendaji wa kazi zangu za kila siku, kama kiongozi ninajukumu la kusimamia dira ya taasisi yetu ili itambulike kimataifa katika kutoa huduma, mafunzo na utafiti wa moyo”alisema Dkt. Tulizo Shemu Mkururugenzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group.

“Ili tuweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa tunahitaji kuwa na timu imara na yenye nguvu na kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano, ninaamini haya tunayojifunza leo yataongeza ufanisi katika kazi zetu za kila siku”, alisema Dkt. Angela Muhozya Mkurugenzi wa Upasuaji.

Dkt. Angela alisema wamefundishwa jinsi ya kuwa wazalendo kwa nchi yao na wagonjwa wanaowahudumia na kutumia vizuri rasilimali za Serikali.