JKCI yaandaa mpango mkakati utalii tiba July 29, 2025
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Jul 30, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yaandaa mpango mkakati wa utalii tiba wa kuhakikisha tiba utalii Tanzania inashika hatamu kwa kutumia teknolojia katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.
Mpango mkakati huo ulioandaliwa kwa siku tatu na wajumbe wa kamati ya utalii tiba wa Taasisi hiyo umelenga kuitikia wito wa Mhe. Rais Dkt. Samia Sululhu Hassan kuhakikisha tiba utalii Tanzania inakuwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mwenyekiti wa kamati ya utalii tiba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Harun Nyagori alisema wajumbe hao wametumia siku tatu kukaa pamoja na kuandaa mpango ambao utatoa muongozi katika kuwahudumia wagonjwa wanaotoka nchi mbalimbali kutibiwa JKCI.
“Mpango mkakati huu tunaouandaa upo katika hatua ya kwanza, ukishapitishwa utatoa muongozo wa namna ya kupata soko la wagonjwa kutoka pembezoni na karibu na mipaka inayizunguka Tanzania lakini pia kutoka maeneo mengine duniani kutibiwa katika Taasisi yetu”, alisema Prof. Nyagori
Prof. Nyagori aliushukuru uongozi wa Taasisi hiyo kuiamini na kuiwezesha kamati ya utalii tiba kutengeneza mpango mkakati wa utalii tiba wa kwanza utakaosimamia shughuli zote za utalii tiba katika Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa kuandaa mpango mkakati wa utalii tiba wa Taasisi hiyo Sylvester Nandi alisema JKCI imewekeza katika miundombinu na wataalamu hivyo kama watafuata muongozo uliopo katika mpango mkakati huo utalii tiba nchini utakuwa.
Nandi alisema baada ya kukaa na wajumbe wa kamati ya utalii tiba wa JKCI ameweza kuona na kuifahamu zaidi Taasisi hiyo ambayo inatoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa.
“Kwa kipindi cha siku tatu nimekaa na wataalamu kutoka JKCI kuandaa mpango mkakati wa utalii tiba ambapo kwa pamoja tumepitishana katika maeneo mbalimbali na kuweka mikakati ambayo ikifuatwa itakuza utalii tiba nchini”, alisema Nandi