Watu 506 wapimwa moyo Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Jul 03, 2025
Watu 506 wamepata huduma ya uchunguzi wa moyo bila malipo katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika jana katika Viwanja vya ChinangalI Park jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya upimaji waliyoitoa katika Maadhimisho hayo.
Dkt. Maucky alisema kati ya watu waliowapima 306 sawa na asilimia 60 walikuwa na matatizo mbalimbali ya moyo yakiwemo ya shinikizo la juu la damu, mfumo wa umeme wa moyo, mishipa ya damu kuziba na valvu kutokufanya kazi vizuri.
“Watu 291 tuliwafanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi ambapo watu 22 tuliowakuta na matatizo ya moyo yaliyohitaji uchunguzi zaidi na matibabu ya kibingwa tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”.
“Kuna ambao tumewakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu hawa tumewapa ushauri wa aina gani ya dawa za kutumia ambazo zitawasaidia pia tumewapa ushauri wa kufuata mtindo bora wa maisha”, alisema Dkt.Maucky.
Dkt. Maucky alitoa wito kwa wananchi kufuata matumizi sahihi ya dawa wanazoandikiwa na wataalamu wa afya kwani kuna baadhi ya watu waliokutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu walikuwa wameacha kutumia dawa kwa muda mrefu bila sababu za msingi.
Naye mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo alisema watu walioonwa katika banda hilo walipewa ushauri wa lishe bora na kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo.
“Asilimia 90 kati ya watu 195 niliowapa ushauri wa mtu mmoja mmoja walikuwa na uzito mkubwa ukilinganisha na urefu wao nimewashauri vitu vya kufanya ikiwemo aina ya vyakula ambayo watavitumia pamoja kufanya mazoezi ili wapunguze uzito”.
“Ni muhimu watu wakafuata mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kutotumia bidhaa aina ya tumbaku na kutokunywa pombe kupitiliza kwa kufanya hivi wataweza kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, alisema Lingindo.