Waziri Mkuu Majaliwa aishauri JKCI kufungua matawi nje ya nchi
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Jun 19, 2025
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa aishauri Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuangalia uwezekano wa kufungua matiwi ya Taasisi hiyo nje ya nchi.
Hayo ameyasema leo alipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha, jijini Arusha.
Mhe. Majaliwa alisema JKCI sasa inafanya vizuri na imesaidia kuipunguzia Serikali gharama ya kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi kwani sasa huduma nyingi za matibabu ya moyo zinapatikana hapa nchini.
“Hongereni sana kwa huduma nzuri mnayoitoa kwa wagonjwa wa moyo, JKCI sasa ni jicho la nchi katika masuala ya matibabu ya moyo kwa kuimarisha huduma zake na kuwapa unafuu wagonjwa wa moyo kupata huduma kirahisi, angalieni namna ya kupeleka huduma hizi nje ya mipaka ya Tanzania kwa kufungua matawi yenu”, alisema Mhe. Majaliwa
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema Taasisi hiyo imefanikiwa kufanya tiba utalii kwa kufanya kambi maalumu za matibabu ya moyo katika nchi za Comoro, Malawi na Zambia.
“Taasisi yetu imekuwa ikiwafikia wananchi wengi katika mikoa mbalimbali nchini kwa kufanya kambi maalumu za matibabu ya moyo pia tumeweza kuvuka mipaka ya Tanzania lengo likiwa kuimarisha tiba utalii nchini”, alisema Dkt. Waane
Dkt. Waane alisema Taasisi hiyo pia imeweza kuwasogezea huduma karibu wananchi kwa kufungua matiwi yake maeneo maeneo ya Kawe ili kuwapunguzia msongamano wa kupata huduma za matibabu ya moyo katika eneo moja.
Kwa kipindi cha miaka mnne Taasisi hiyo imeweza kuwapatia matibabu wagonjwa 689 kutoka nje ya nchi zikiwemo nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Nigeria, Siera Leon, Zimbambe, Zambia, Uganda, Congo, Ethiopia, Burundi, na wengine kutoka nje ya Afrika katika nchi za Armenia, china, Ujerumani, India, Norway, Ufaransa na Uingereza.