Vijana wa Fountain Gate Academy kupimwa moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Jun 19, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Klabu ya Fountain Gate Academy na Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (TMSA) wasaini makubaliano kuanzisha na kusimamia programu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo wa academy hiyo.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo jana jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema makubaliano hayo yamelenga kufanya uchunguzi wa awali wa moyo kwa wachezaji wa Fountain Gate FC pamoja na wanafunzi wa shule 15 zinazomilikiwa na Academy hiyo.
“Makubaliano haya yatatoa fursa kwa wanafunzi wa Fountain Gate waliopo katika shule 15 zilizopo mikoa mbalimbali ya Tanzania wanaoshiriki katika shughuli za michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema mpango huo wa kuanzisha sports cardiology program inayohusisha pre-participation cardiac screening kwa wanamichezo ni hatua muhimu katika kuhakikisha usalama wa wanamichezo nchini.
“Lengo letu ni kubaini mapema matatizo ya moyo ambayo yanaweza kuwa hatari na yasiyoonekana kwa macho ili kuyazuia kabla hayajasababisha madhara makubwa”,
“Hii ni pamoja na kuzuia vifo vya ghafla vya moyo (sudden cardiac death), ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa duniani kote kwa wanamichezo, hata wale waliokuwa wakionekana kuwa na afya njema”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fountain Gate Academy Japhet Makau alisema Taasisi hiyo imepata fursa ya kushirikiana na JKCI kulinda afya za wachezaji wake na kuwaweka watoto katika mikono salama kwa kuwafanyia vipimo vya moyo kabla ya kuingia kwenye michezo.
Makau alisema Taasisi yake inaamini JKCI itaondoa hofu kwa wachezaji wakati wapo uwanjani na kuwajenga vijana kujiamini hivyo kuongeza nguvu katika michezo yao.
Progamu hiyo mpya na ya kipekee ni sehemu ya upanuzi wa huduma za kinga inayofanya na JKCI katika jamii, na kuelekeza nguvu katika kuzuia vifo vya ghafla vya wanamichezo hasa kwa vijana wanaoshiriki michezo.
Programu hiyo imesainiwa mara baada ya JKCI kusaini mkataba na Shirika la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) hivi karibuni wakiwa na lengo la kuwalinda wachezaji na madhara yanayoweza kujitokeza pindi wanapokuwa uwanjani.