• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Waziri Simbachawene aipongeza JKCI kwa matibabu bure ya moyo Dodoma

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jun 19, 2025
image description

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.

 Pongezi hizo amezitoa jana alipotembelea banda la taasisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

 Akiwa katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Mhe. Simbachawene aliona huduma za ushauri, upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wananchi pamoja na vifaa visaidizi vya moyo ambavyo wanawekewa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji na vifaa vinavyotumika katika upasuaji wa moyo.

 “Ninawapongeza kwa huduma mnayoitoa ya kuokoa maisha ya wananchi wenye shida za moyo, ninawasihi  muendelee na moyo wenu wa kujitoa ili watu wengi zaidi wafikiwe na hudum hii na kupata matibabu mapema”, alisema Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha alisema huduma wanazozitoa katika maonesho hayo ni upimaji wa shinikizo la damu (BP), upimaji wa kiwango cha sukari kwenye damu, upimaji wa uwiano baina ya urefu na uzito, vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi.

“Pia tunatoa ushauri wa kiafya kuhusiana na magonjwa ya moyo, elimu ya lishe, elimu ya upasuaji wa moyo, elimu ya upandikizaji wa vifaa visaidizi vya moyo, elimu ya uzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo na huduma ya utumishi na utawala”.

“Huduma hizi tunazitoa bila malipo yoyote yale, ninawaomba wananchi mtembelee banda letu ili muweze kupata huduma huduma za elimu, ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo”,  alisema Ghati.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Himiza matumizi ya mifumo ya kidigilali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji”.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kuwafuata wananchi mahali walipo ambapo hadi sasa wameshafika zaidi ya mikoa 20 na kuhudumia watu zaidi ya 21,324.