• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI yawapa siku nane wananchi Dodoma kupima moyo bure

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jun 19, 2025
image description

 Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watashiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa huduma za kibingwa za  uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi  hiyo Dkt. Angela Muhozya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma  tarehe 16 hadi 26 mwezi huu.Dkt. Angela alisemma huduma hiyo itatolewa bila malipo yoyote ambapo wananchi watapata huduma za upimaji na matibabu ya  magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.

 “Tutatoa huduma za ushauri wa kiafya kuhusiana na magonjwa ya moyo, elimu ya lishe bora, elimu ya upasuaji wa moyo, elimu ya upandikizaji wa vifaa visaidizi vya moyo, elimu ya uzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo na huduma ya Utumishi na Utawala”.

“Wagonjwa watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapo hapo na wale watakaokutwa na matatizo yatakayohitaji matibabu ya kibingwa watapewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”, alisema Dkt. Angela.

Dkt. Angela alisema kupitia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema; “Himiza matumizi ya mifumo ya kidigitali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji”, wataonesha wananchi namna ambavyo wanatumia  mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma za kibingwa  za matibabu ya moyo ndani na nje ya nchi.

 “Ninawaomba wananchi wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani mtembelee katika banda letu na kupima  afya zenu kwa kufanya hivi mtaweza kujua kama mna matatizo ya moyo na hivyo  kuanza matibabu mapema kwa atakayegundulika kuwa mgonjwa”.

 “Pia ukifika katika banda letu utafahamu  namna ambavyo Taasisi yetu inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete  ya mwaka 2015, kupitia Tangazo la Serikali Na. 454 la mwaka 2015”, alisema Dkt. Angela.