Rais Dkt. Samia aipongeza JKCI kwa kuwafuata wananchi mahali walipo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Jun 19, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo bila malipo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.
Pongezi hizo amezitoa jana wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Dkt. Samia alisema taasisi ambazo zinatoa huduma ya kuisaidia jamii kama ambavyo JKCI inafanya zinatakiwa kupongezwa na kutambuliwa kwa mchango wao wanaoutoa.
“Taasisi ambazo zinatoa mchango wao kwa jamii kutokana na huduma wanazozitoa nazo zinatakiwa kuonekana na kuonesha wanachangia kiasi gani kwa umma kama ambavyo wanafanya JKCI kwani mchango wa JKCI ni mkubwa na unaifikia jamii”, alisema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetoa gawio la shilingi Bilioni 2 kupitia huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi 27,600 katika mikoa 16 nchini.
Mchechu alisema kupitia jukwaa la kutathmini, kutafakari, kusherehekea mafanikio, kusisitiza uwekezaji na uwajibikaji katika utumishi wa umma wameona umuhimu wa kuitambua Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutokana na mchango wake katika jamii kupitia kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba.
“JKCI hata tusipowasoma kwenye pesa tunawasoma kwenye mafanikio yao, huduma ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wanayoifanya tumeshuhudia imefika katika mikoa 16 ambapo watu 27,600 wameweza kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Mchechu.
Aidha Mchechu alisema kwa mara ya kwanza JKCI imeonekana ikitoa huduma katika Kliniki zake zilizopo nje ya makao makuu, hali inayoonyesha mafanikio na ukuaji mkubwa wa Taasisi hiyo nchini.
“Sasa hivi ukitaka kutibiwa JKCI unaweza kwenda kwenye matawi yake yaliyopo Oysterbay, Kawe, Dar Group Hospitali na tawi lake lingine lililopo Arusha AICC”, alisema Mchechu”, alisema Mchechu.
Mchechu alisema kama Ofisi ya Msajili wa Hazina itaangalia namna ya kuhakikisha mafanikio na ukuaji wa biashara unaofanywa na JKCI unarudi na kuwagusa watendaji wa Taasisi hiyo ili kulete chachu kwa watu wengine kufanya kazi kwa bidii, kugusa watu wengine na mwisho waweze kugusa maisha yao.